Plus 255 Studios

Plus 255 Studios
Home » » LIWALE; KUWAPIGA HAWA SIO SURUHISHO

LIWALE; KUWAPIGA HAWA SIO SURUHISHO

Liwale. Polisi mkoani Lindi inawashikilia watu 50 ikiwatuhumu kujihusisha na vurugu zilizotokea juzi usiku wilayani Liwale, Lindi na kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi.
Ghasia hizo zilizozuka juzi katika Kijiji cha Liwale B na kusababisha kuteketezwa kwa mali nyingi, wizi, uharibifu pamoja na kuuawa kwa mifugo, zilitokana na wakulima kudai kupunjwa fedha zao za korosho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga alisema jana kuwa licha ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao, polisi pia imekamata vitu mbalimbali vilivyoporwa ambavyo alivitaja kuwa ni pamoja na mabati, nondo na vifaa vilivyoporwa wakati wa vurugu hizo.
Wakulima wa korosho wanadaiwa kuanzisha vurugu hizo wakitaka kulipwa nusu ya mwisho ya fedha zao za korosho walizouza katika Chama cha Ushirika Mnali kwa Sh1,200 lakini uongozi wa chama hicho ukapanga kuwalipa Sh200.
Akizungumzia sababu ya kulipa kiasi hicho kidogo, Katibu wa chama hicho, Juma Majivuno alisema: “Biashara haikwenda vizuri kutokana na kuporomoka kwa soko la korosho, ndiyo maana tukawaambia tutawalipa Sh200 lakini wakakataa wanataka tuwalipe fedha zote Sh600, sasa sisi hatuna hizo fedha.”
Kamanda Mwakajinga alisema watuhumiwa hao ambao bado wanashikiliwa na polisi, watafikishwa mahakamani mara moja huku akiwataka wananchi kuondoa hofu na kuendelea na kazi zao akisema hali sasa ni shwari.
Mbunge alia na siasa
Akizungumza baada ya kukagua mabaki ya nyumba yake iliyoteketea kwa moto, Mbunge wa Liwale (CCM), Faith Mitambo alisema kuwa tukio la uharibifu wa mali lililofanywa na makundi ya vijana halikutokana na madai ya korosho, bali ni masuala ya kisiasa.
“Haya ya korosho ni kama njia tu, hapa zimetumika siasa... kuna mkono wa siasa hapa... kama si siasa ni nini! Kwa nini walioathiriwa ni wanachama wa CCM tu?”
Mbunge huyo alichomewa nyumba zake mbili, huku moja ikiteketea kabisa. Wengine waliochomewa nyumba zao ni Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Umoja, Hassan Myao na Makamu wake, Hassan Mpako, Diwani wa Viti Maalumu CCM Liwale, Amina Mnocha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Abbas Chigogola, Mwenyekiti wa CCM Wilaya Liwale, Mohamed Ng'omambo na Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya Liwale, Abdallah Chande.
Nyumba zaidi ya 20 nyingi zikiwa za viongozi wa CCM na vyama vya msingi, ziliteketezwa kwa moto.
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa ilikutana jana kutwa nzima chini ya Mwenyekiti wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Abdallah Ulega kutathmini athari iliyotokana na vurugu hizo.

0 comments:

Post a Comment