Rasimu ya Katiba iliyotolewa hivi karibuni na Tume ya Katiba imetoa mapendekezo ya kuwepo kwa Muungano wa Serikali Tatu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph
Warioba, Serikali ya Muungano iliyokuwa ikisimamia mambo 22 sasa
itabaki na mambo saba, huku mengine yakirudishwa kwenye Serikali za
Zanzibar na Tanzania Bara.
Amedokeza kuwa mbali na Serikali tatu, wapo wananchi waliotaka Serikali moja, mbili, nne na wengine Muungano wa Mkataba.
Kwa maoni yangu Tume ya Katiba imethubutu
kusikiliza kilio cha wengi waliokuwa wakiukosoa Muungano. Ni jambo
ambalo Chama Cha Mapinduzi hakikupenda kuvunja mwiko, ndiyo maana
kinasisitiza Serikali Mbili.
Mimi naamini kabisa, kwa jinsi Mwalimu Nyerere
alivyokuwa na misimamo yake, angekuwa hai leo, asingekubaliana na rasimu
hii ya Katiba.
Asingekubali kuona Muungano aliouasisi ukiwa hatarini kuvunjwa kwa kuwaridhisha wanaotaka Serikali Tatu.
Tukiangalia chanzo cha Muungano wetu, utaona
sababu nyingi, lakini ya msingi ni ya usalama. Ni kweli kuna wanaosema
watu wa Tanganyika na Zanzibar wana undugu, lakini hii haina mashiko
kwani hata ukiangalia nchi zote zilizotuzunguka tuna undugu kwa njia
moja au nyingine, mbona hatuungani?
Wengine wanahusisha Muungano na vita baridi kati
ya Urusi na Marekani miaka ya 1980. Inawezekana, lakini mbona vita hiyo
ilipoisha Muungano huo haukuvunjika.
Kwa hiyo, sababu kubwa Muungano wetu ni usalama.
Baada ya kupata uhuru mwaka 1961, Mwalimu Nyerere kama viongozi wengine
wa Afrika walitafuta njia za kulinda mamlaka yao kwa namna yoyote ile.
Kwa Nyerere, Zanzibar ilikuwa tishio siyo la
utawala wake tu, bali kwa Tanganyika nzima. Ndiyo maana aliwahi
kukaririwa akisema, angetamani Tanganyika ivimeze visiwa hivyo au
avisogeze mbali kabisa na eneo lake.
Kumbuka wakati huo tayari kulikuwa na chokochoko
za kisiasa zilizoanza tangu miaka ya 1957 kati ya vyama vya ASP, ZNP,
ZPPP na Umma.
Mwalimu alihofu kuwa vurugu hizo zingeambukiza
wanasiasa wa bara au hata maadui wa nje kuvitumia visiwa hivyo
kushambulia Tanganyika.
0 comments:
Post a Comment