Dodoma. Mvutano kati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila umechukua sura mpya baada ya mwanasheria huyo kugoma kupatanishwa huku akitishia ‘kumshughulikia’ mbunge huyo.
Ugomvi baina yao uliendelea jana asubuhi nje ya
Ukumbi wa Bunge muda mfupi baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuahirisha
kikao cha Bunge hadi leo.
Licha ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu
kumwita Jaji Werema na Kafulila akiwataka kupeana mikono kama ishara ya
kuzika tofauti zao, Jaji Werema alikataa na nusura amvamie mbunge huyo.
Juzi asubuhi baada ya Zungu kuahirisha kikao cha
Bunge, muda mfupi baada ya Jaji Werema na Kafulila kurushiana maneno
bungeni, mwanasheria huyo alitaka kumtia adabu Kafulila kwa kumwita
mwizi.
Kafulila alimwita Jaji Werema mwizi akijibu mapigo baada ya awali kuitwa tumbili na mwanasheria huyo.
Ilivyokuwa jana
Wakati akizungumza na gazeti la mwananchi mara baada ya
Bunge kuahirishwa jana, Jaji Werema alikutana uso kwa uso na Kafulila
katika Viwanja vya Bunge na kuanza kumlalamikia mbunge huyo kwa kitendo
chake cha kumwita mwizi.
“Unamuona huyo jana (juzi), aliniita mimi mwizi.
Yaani mtu mzima kama mimi naitwa mwizi, kwa kweli sikupendezwa kabisa na
kauli yake,” alisema Jaji Werema huku akimfuata Kafulila ambaye
alitembea harakaharaka kumkwepa mwanasheria huyo.
Jaji Werema alisema juzi alishikwa na jazba baada
ya kuitwa mwizi lakini akasema hakuwa na nia ya kumpiga ndani ya Ukumbi
wa Bunge.
Wakati Jaji Werema akiendelea kumlalamikia
Kafulila, alitokea Zungu na kumtaka mwanasheria huyo kumsamehe mbunge
huyo... “Mheshimiwa naomba mpeane tu mikono kama ishara ya kusameheana,
yale mambo ya jana (juzi) yamekwisha.”
Lakini badala ya kukubaliana na ombi la Zungu,
Jaji Werema alihamaki huku akitaka tena kumvamia Kafulila... “Mimi
nakwambia Kafulila nitakukata kichwa, we subiri tu labda ukiniomba
msamaha.”
Kafulila naye alijibu mapigo... “Huwezi kunikata kichwa Werema, huwezi, yaani uniue, hapana huwezi tena nakwambia huwezi.”
0 comments:
Post a Comment