Plus 255 Studios

Plus 255 Studios
Home » » Tanganyika kuwamo ndani ya Katiba ya Muungano bila Zanzibar ni kuua Muungano

Tanganyika kuwamo ndani ya Katiba ya Muungano bila Zanzibar ni kuua Muungano



Kwa ufupi
Katika Muungano wowote wa nchi, isipokuwa ule wa Serikali moja, huwa ni lazima kuwe na mgawanyo wa kimamlaka baina ya mambo ya muungano na mambo yasiyo ya muungano. Mamlaka hizi kidesturi, kikatiba, kisera, kisheria na kiutendaji, ndiyo huwa zimepewa dhamana ya kusimamia au mambo ya muungano ama mambo yasiyo ya muungano.
Baadhi ya viongozi watambue Tanganyika siyo Jamhuri ya Muungano

Hali ikoje sasa
Leo nijikite katika kuongeza uelewa juu ya tofauti iliyopo kati ya mambo ya muungano na yasiyo ya muungano. Nchi yetu inatokana na muungano wa zilizokuwa nchi mbili huru kwa maana ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo ziliwezesha kuundwa kwa nchi mpya, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika Muungano wowote wa nchi, isipokuwa ule wa Serikali moja, huwa ni lazima kuwe na mgawanyo wa kimamlaka baina ya mambo ya muungano na mambo yasiyo ya muungano. Mamlaka hizi kidesturi, kikatiba, kisera, kisheria na kiutendaji, ndiyo huwa zimepewa dhamana ya kusimamia au mambo ya muungano ama mambo yasiyo ya muungano.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, tuna mamlaka tatu, moja ni mamlaka inayosimamia mambo ya Muungano, mbili, ni mamlaka inayosimamia mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara (Tanganyika) na tatu ni Mamlaka inayosimamia Mambo yasiyo ya Muungano ya Zanzibar.
Kikatiba kila Mamlaka huwa na vyombo vinavyopewa dhamana ya kutekeleza majukumu ya kiutendaji (Serikali), majukumu ya kutunga sheria (Bunge au Baraza) na majukumu ya kutoa haki (Mahakama). Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza mamlaka ya mambo yasiyo ya Muungano ya Zanzibar, kiutendaji yanatekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Serikali ya Muungano imepewa dhamana ya kutekeleza mambo ya Muungano na mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara.
Kama kila kitu kingekuwa kinatekelezwa sawasawa katika utaratibu huu, tusingekuwa na madai yasiyoisha kutoka Zanzibar hasa kutoka katika Baraza la Wawakilishi na SMZ kwa jumla. Sote tu mashahidi zinazoitwa kero zimekuwa ndiyo mjadala mkubwa katika medani za kisiasa hasa linapozungumzwa suala la muungano. Utafiti ambao ulifanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba umedhihirisha kwamba changamoto zinazouandama Muungano ni zaidi ya 40.
Ukiacha lugha ya kero na changamoto, yako pia manung’uniko ambayo kila upande wa Muungano unayo na siyo manung’uniko madogo au ya kuyapuuzwa. Kitendo cha Serikali ya Muungano kushughulika na mambo ya Muungano pamoja na yale ya Tanzania Bara kinatamkwa na wengi, hasa kutoka upande wa Zanzibar kuwa ndiyo mzizi wa tatizo. Tume ya Pamoja ya Fedha, nayo ilipewa kazi ya kuchanganua na kupambanua matumizi halisi ya Serikali ya Muungano ukitoa yale ya upande wa Tanzania Bara. Msingi wa kuchambua gharama na matumizi ilikuwa kuweza kuweka utaratibu bora wa kutekeleza mambo ya Muungano, lakini pia namna bora ya kuchangia gharama za Muungano hasa kutoka Zanzibar.
Kazi ya Tume imefanyika hadi masharti ya kikatiba yakawekwa katika Katiba ya Muungano, yanayoelekeza kuanzishwa kwa akaunti ya fedha ya pamoja katika Ibara ya 133. Jambo hili halijafanyiwa kazi tangu lilipowekwa kwenye Katiba miaka 30 iliyopita na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali miaka 13 iliyopita.
Kwa vile akaunti haijaanzishwa na hakuna anayeonekana kuelewa umuhimu wa kutenganisha gharama za kuendesha mambo ya Muungano pekee mbali na gharama za jumla zinazoihusisha mamlaka ya Tanzania Bara, matokeo ni Zanzibar kukataa kabisa kuchangia gharama za Muungano kwa takriban miaka 30 sasa na Tanzania Bara ndiyo imejikuta ikibeba gharama za muungano peke yake.
Tunayopaswa kuyajua na kubadilika mapema
Fikra ya kwamba kila la Tanganyika linapaswa liwe chini ya Muungano ni fikra potofu na ambayo haitaarifiwi kwa uhalisia wa zinazoitwa kero na changamoto za Muungano. Hivi, tukizingatia utaalamu na siyo hisia, je, kuna sauti kubwa zaidi kutoka Zanzibar zaidi ya Kamati ya Makatibu Wakuu wa SMZ? Kamati ya Makatibu Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi wanataka mambo machache ya Muungano na Muundo wa Serikali Tatu. Tafsiri ya wanachokitaka ni Tanganyika pia kuwa na mambo yake yasiyo ya Muungano yaliyotenganishwa na yale ya Muungano. Kwa maneno mengine, Wazanzibari na Watanganyika kwa hoja na sababu zenye mashiko, walitaka mambo ya Tanganyika yasimamiwe na vyombo vya Tanganyika kama ilivyo kwa Zanzibar leo.

Kuna baadhi ya viongozi wameendelea kushupaa kwa kudai Rasimu inapaswa izungumze mambo ya wananchi kama vile maji, kilimo, uvuvi, ufugaji, miundombinu na kadhalika. Najiuliza mambo haya viongozi hawa wanasemaje, wanatambua kwa kuyaweka katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano yatakuwa na manufaa kwa wananchi wepi? Je, wamewahi kujiuliza kama wanaposema wananchi huwa wanamaanisha na Watanzania waishio Zanzibar?
Kitendo cha Zanzibar kutaka mamlaka zaidi kwa mambo yao yasiyo ya Muungano kunaiacha Jamhuri ya Muungano ikibaki na kila kitu cha Tanganyika bila ya chochote cha Zanzibar, isipokuwa suala la Ulinzi na Usalama. Wazanzibari wanatupa somo kila siku ila hatujifunzi, tunapuuza, tumekaa kimya na tumeshupaa. Hebu chukulia mifano ifuatayo;
Juzi nimemsikia Mwenyekiti mmojawapo wa Kamati ya Bunge Maalumu akisema kwa sababu ya tatizo la rushwa ufike wakati Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takukuru) iwekwe kwenye Katiba. Nikajiuliza aliposema Takukuru iwekwe kwenye Katiba alijua kwamba Takukuru inafanya kazi Tanzania Bara peke yake? Na je, alijiuliza kwa kuweka mambo mengi zaidi ya Tanganyika katika Katiba tunaifanya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuwa ndiyo Katiba halisi ya Tanganyika?
Kwa maneno mengine kwa mwendo huu tunaandika Katiba ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya Tanganyika na Wazanzibari watashughulika na Katiba yao kwa mambo yao yasiyo ya Muungano.
Hii inamaanisha kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa ni kwa Tanganyika pekee na ile ya Mapinduzi kwa Zanzibar pekee. Je, tunapofika hapo tunajenga Muungano au tunaudhoofisha? Je, hatuwezi kujiuliza kwa nini kila tunapokuwa na chombo cha kufanya kazi cha Muungano au kinachobeba haiba ya Muungano, Zanzibar huenda na kuanzisha chombo hicho?
Hebu angalia tena mifano kadhaa hapa: Kwanza, Tanzania ina Shirika la Viwango nchini (TBS) linaloanzishwa na Sheria namba 2 ya 2009 (Standards Act no. 2 of 2009) na katika kifungu cha 3(2) sheria hii inaeleza; ‘The Bureau shall be the custodian and an overseer of observance of standards in Tanzania’, maana yake TBS itakuwa na dhamana ya kusimamia viwango katika Tanzania (Tafsiri ni yangu). Sasa kama Tanzania kwa mujibu wa Ibara ya 2 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano eneo lake ni Tanzania Bara na Zanzibar. Kwa nini Zanzibar imekwenda na kutunga sheria ya kuanzisha Shirika la Viwango la Zanzibar kwa sheria namba 1 ya Mwaka 2011 kwa Kiingereza; ‘The Zanzibar Standards Act of 2011?’ Katika sheria hii, kifungu cha 2 kinasema sheria hii itatumika kwa bidhaa zinazozalishwa au zinazoingizwa Zanzibar. Sasa chukua muda ujiulize swali, ile TBS ya Ubungo ni ya Tanzania kweli au ya Tanganyika?
Tuutazame mfano wa pili. Kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Tanzania ‘Food, Drugs and Cosmetics Act no. 1 of 2003’, kinaanzisha Mamlaka ya Chakula Dawa na kwa kifupi TFDA. Mamlaka hii imepewa dhamana ya kushughulikia kisheria masuala yote ya uhusiano viwango na usalama wa vyakula, dawa, dawa asilia, vifaa tiba, sumu na vipodozi nchini. Kama hii haitoshi, Zanzibar pia imeanzisha ‘Zanzibar Food and Drugs Board’ kwa sheria ya Baraza la Wawakilishi mwaka 2006, ambayo imepewa masuala yale yale. Najiuliza, kwani hii TFDA ni ya Tanzania kweli? Kama siyo, kwa nini inabeba haiba ya Taasisi ya Muungano? Lakini, kabla sijajijibu mwenyewe, tafakari ujumbe unaotumwana Serikali ya Zanzibar mara kwa mara kila ufanyikapo uamuzi katika Muungano kwa Watanganyika waliovaa kanzu ya Muungano.
Twende kwenye mfano wa tatu.Mwenyekiti wa Kamati mojawapo ya Bunge Maalumu aliyetaka TAKUKURU iwekwe katika Katiba, je, alizingatia Kifungu cha 2(1) cha Sheria ya Kupambana na Rushwa Sura ya 329 kinachosema bayana mamlaka ya Sheria hii na Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takukuru) inafanya kazi Tanzania Bara peke yake wakati kule Zanzibar kuna sheria maalumu kabisa, Sheria ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi namba 1 ya Mwaka 2012. Sasa kama Tanganyika ina Takukuru yake na Zanzibar wana Taasisi yao ya Kupambana na Rushwa, kwa nini Tuweke Takukuru kwenye Katiba ya Muungano?
Tuendelee na mfano wa nne, Tanzania tunalo Baraza la Mitihani la Taifa linaloanzishwa na ‘The National Examinations Council of Tanzania Act CAP 107’, miaka nenda rudi. Tunajua Baraza hili ni la Tanzania, sasa mbona Zanzibar imeunda kwa sheria ya Baraza la Wawakilishi chombo kinachoshughulika na viwango vya elimu na tathmini kwa Zanzibar yaani ‘The Zanzibar Educational Measurement and Evaluation Council Act no. 6 of 2012’. Hivi bado wale wanaotaka mambo ya Tanganyika yawekwe kwenye Katiba ya Muungano halafu yale ya Zanzibar yakae kwenye Katiba ya Zanzibar unauona Muungano ukiimarika hapo?
Rasimu inapendekeza nchi moja ambayo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye Muundo wa Shirikisho lenye Mamlaka Kamili na lenye Serikali 3. Katika muundo huu Serikali ya Muungano itakuwa ndiyo inajukumu la kushughulikia mambo ya Muungano lakini pia Serikali ya Muungano kupitia Tume yake ya Uhusiano na Uratibu itakuwa na jukumu kwa mujibu wa ibara ya 111(1)(b) la kusimamia, kuratibu na kuhakikisha kwamba kuna kuwiana kwa sera na sheria za nchi washirika katika mambo yasiyo ya Muungano.
Wito wangu, tuitazame Rasimu kwa jicho chanya na kwa hakika tunaiona Jamhuri ya Muungano Mpya ambayo ni imara, yenye nguvu zaidi na itakayotupeleka zaidi ya miaka 50 ijayo. Tusishupae tukashindwa kuwa waungwana tukapitwa na mazuri na mema ya nchi, ambayo Rasimu inayo na kama ambavyo Watanzania kwa hoja na sababu walitaka iwe.
Tuonane wiki ijayo.

0 comments:

Post a Comment