Plus 255 Studios

Plus 255 Studios
Home » » RASIMU YA KATIBA YA PILI NA MAJIBU KWA CHANGAMOTO ZOTE ZA SERIKALI 3

RASIMU YA KATIBA YA PILI NA MAJIBU KWA CHANGAMOTO ZOTE ZA SERIKALI 3

 

RASIMU YA KATIBA TOLEO LA PILI ILISHATOA MAJIBU KWA CHANGAMOTO ZOTE ZA SERIKALI 3

NINAANDIKA KAMA SEHEMU YA KUONDOA HOFU KWA WALE WENYE HOFU

Hofu iliyozungumzwa juu ya Serikali 3 haina mashiko na ni ya kufikirika zaidi

Leo nimeona nifafanue hii sintofahamu kuhusu changamoto za Muundo wa Serikali Tatu. Kimsingi muundo huu ukiacha ukweli kwamba wananchi wameutolea maoni, kwa hoja na sababu lakini pia Tume ya Katiba iliufanyia utafiti, ikazingatia uhalisia wa historia na uhalisia wa utendaji katika mazingira ya sasa. Kwa unyenyekevu mkubwa nieleze changamoto zilizoibuliwa na Taarifa ya Utafiti juu ya Masuala ya Muungano na nieleze majibu ambayo Rasimu imeyatoa kwa umakini mkubwa. Majibu ninayoyatoa hapa yametolewa pia katika Ripoti ya Tume juu ya Mchakato wa Katiba Mpya. Nitoe rai watu kuzungumza changamoto za muundo huu na kuona ni mapendekezo gani yametolewa kukabiliana na changamoto hizo. Naomba usomapo Makala hii fanya rejea kwenye Rasimu ya Katiba Toleo la Pili.

Changamoto hizo ni kama ifuatavyo;

1.   Muundo huu unaweza ukawa na gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma;

Muundo unaopendekezwa katika Rasimu hauna gharama kwasababu zifuatazo kwa ufupi;

(i)   Mambo ya Muungano ni Machache, yamepungua kutoka 22 hadi 7, Ibara ya 63
(ii)  Mambo ya yasiyo ya Muungano sasa yatatekelezwa na Tanganyika na Zanzibar Ibara ya 64
(iii)Serikali ya Jamhuri ya Muungano ni ina Mamlaka Makubwa ila ndogo, Mawaziri wake hawatozidi 15, Ibara ya 98
(iv)Bunge la Jamhuri ya Muungano lina Mamlaka Makubwa lakini ni dogo, Wabunge jumla ni 75, Ibara ya 113
(v)  Utaratibu mzuri wa kuhakikisha kunakuwepo na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma soma ibara za 227, 228, 229 na 232

2.   Muundo huu unaweza kuibua tatizo la uchangiaji gharama za uendeshaji wa muungano baina ya washirika;

Rejea Majibu ya Rasimu kwa suala hili hapa kwa ufupi;

(i)   Kwanza itambulike, suala la uchangiaji ni la Kikatiba, sio takwa la mtu, utashi wa kiongozi au maamuzi ya Serikali ya Tanganyika au Zanzibar. Ambaye atakataa kuchanga ama Rais wa Tanganyika au Zanzibar anahatarisha uwepo wa mamlaka ya Jamhuri ya Muungano na anataka kutweza mamlaka ya muungano, huyo ni mhaini kwasababu aliapa kuutetea na kuudumisha Muungano, rejea Ibara ya 9, 69 na 88(2)(d)

(ii)  Masuala ya uchangiaji wa gharama za uendeshaji wa muungano, ni masuala ya kiutaalamu, kiutendaji na kiuongozi. Masuala haya kimfumo yataratibiwa na Tume ya Uhusiano na Uratibu rejea Ibara za 109, 110, 111 na 112

(iii)Ikumbukwe anayetunza akaunti za fedha za Nchi Washirika ni Benki Kuu ya Jamhuri ya Muungano kupitia Benki za Serikali za Nchi Washirika, rejea Ibara ya 233(1)(d) na isome pamoja na Ibara ya 234

(iv)Vyanzo vya Mapato vilivyo ainishwa na Rasimu vinatosha Kabisa kukidhi mahitaji ya Jamhuri ya Muungano na Serikali yake, Michango ni aina moja tu ya vyanzo, viko vyanzo vitano ambavyo kwa tathmini ya Tume vinatosha kabisa, rejea Ibara ya 231

3.   Muundo huu unaweza ukasababisha uwepo wa sera zinazotofautiana au kukinzana juu ya masuala ya msingi ya nchi na hivyo kuleta migogoro kati ya Washirika wa Muungano au baina ya Washirika wa Muungano na Serikali ya Muungano;

Rejea Majibu ya Rasimu hapa kama ifuatavyo;

(i)   Rasimu imefafanua, Mamlaka ya Serikali ya Muungano ambayo yako bayana zaidi tofauti na sasa na hata pale Serikali ya Muungano ikitaka kutekeleza jambo lililo chini ya mamlaka ya Serikali ya Tanganyika au Zanzibar itafanyika hivyo kwa mujibu wa Katiba, rejea Ibara ya 62

(ii)  Rasimu inatoa maelekezo kwa Nchi washirika kuzingatia misingi ya ushirikiano kwa haki na usawa kwa ajili ajili ya ustawi ulio bora wa wananchi kutoka pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano rejea Ibara ya 65(1)

(iii)Rasimu imetatua changamoto tajwa hapo juu kwa kuweka mfumo thabiti kikatiba ambao utakuwa na jukumu la kusimamia, kuratibu na kuhakikisha kuna kuwiana kwa sera na sheria kwa mambo yasiyo ya muungano, rejea Ibara ya 111(1)(b)

(iv)Rasimu pia imeweka Misingi Mikuu ya Maendeleo ya Nchi ambayo inapaswa kuwa ndio Dira ya Taifa na maelekezo kwa Mamlaka ya Nchi. Masuala ya Misingi na Malengo ya Taifa (Dira) usimamizi na uratibu wake uko kitaifa, hapa rejea Ibara za 10, 11, 111(1)(d) na 116

4.   Kuna uwezekano mkubwa kwa muundo huu kuleta tofauti za kimaendeleo baina ya pande mbili za muungano kutokana na uwezekano wa kuwa na sera na mipango tofauti. Uwezekano wa kuwa na tofauti kubwa za kiitikadi na utendaji unaweza kuchangia hali hiyo.

Rejea Majibu ya Rasimu kama ifuatavyo;

(i)   Rasimu imetatua changamoto tajwa hapo juu kwa kuweka mfumo thabiti kikatiba ambao utakuwa na jukumu la kusimamia, kuratibu na kuhakikisha kuna kuwiana kwa sera na sheria kwa mambo yasiyo ya muungano, rejea Ibara za 110 (a)(b)(c) na (d), 111(1)(a)(i)(ii), 111(1)(b) na 111(1)(d)

(ii)  Itikadi inaongozwa na Dira ya Taifa, ni dira ndio inasema ndoto za wananchi na itikadi ni namna ya kufika huko ambako watanzania wanataka kufika. Kidesturi itikadi huwa katika ngazi ya vyama vya siasa. Kwa mara ya kwanza Rasimu inapendekeza Dira ya Taifa Katika Sura ya Pili ya Rasimu ambayo ndio itakuwa ni maelekezo kwa Serikali (ya chama chochote) na Mamlaka zote za nchi, rejea Ibara ya 10, 11, 111(1)(d) na 116

5.   Muundo wa Serikali tatu unaweza ukakuza hisia za utaifa (nationalistic feelings) kwa Washirika wa Muungano na hivyo kufifisha Muungano na kuhatarisha uwepo wake;

Rasimu ililitizama suala hili na yafuatayo ni majibu katika Rasimu;

(i)   Kwanza ifahamike kuwa, uraia ndio msingi mkuu wa uzalendo katika Nchi yoyote. Kama ambavyo mamlaka ya nchi huwa na ukomo katika eneo la kijiografia vivyo hivyo mamlaka ya nchi huwa na ukomo kwa watu inaowajibika kwao, watu hawa hutambulika kwa mujibu wa sheria kama raia. Utaifa wa mtu hujengwa katika uraia, Taifa la Tanzania litajengwa na raia wa Tanzania. Rasimu imependekeza Uraia Mmoja na ni wa Jamhuri ya Muungano na utapatikana kwa njia mbili, kuzaliwa na kujiandikisha, rejea Ibara ya 56

(ii)  Zanzibar na Tanganyika hazina raia wala sio Mataifa, ni maeneo tu ambayo tumeyapa hadhi katika Rasimu ya “Nchi Washirika” na ieleweke Nchi washirika sio Nchi kwa tafsiri ya Sheria za Kimataifa na Rasimu yenyewe. Wanaokaa Tanganyika na Zanzibar sio watanganyika wala sio wazanzibari bali ni wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaoitwa “Watanzania”, rejea Ibara ya 64

(iii)Hisia za utaifa huibuka pale ambapo historia na asili ya wale wanaoungana inapofutwa. Uzoefu umeonesha kuwa kwa kufuta asili na historia ya Tanganyika kwa makusudi ndio umekuwa mwiba mkubwa kwa utangamano na umoja wa Jamhuri ya Muungano. Tanganyika imendelea kujifufua na kujionesha katika nyanja zote kwa sura ya Jamhuri ya Muungano na kuiweka kando Zanzibar kana kwamba ni ka-sehemu ka Tanganyika Mkuu. Salama yetu ni kuiweka Tanganyika kwenye mwanga na kuiwekea masharti ya kikatiba ambayo yataiongoza na kuifanya sehemu na eneo la Nchi Moja inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, rejea Ibara ya 64 na 65

(iv)Mwisho wa siku Tanganyika na Zanzibar si Mataifa, si nchi na hazina raia, Taifa ni Moja, Nchi ni Moja na Raia ni Wamoja na ni wa Nchi inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye Muundo wa Shirikisho lenye Mamlaka kamili na lenye serikali tatu, rejea Ibara za 61, 63, 64, 65, 66, 67, 70, 71, 72, 110, 111,117, 119, 156 na 235

6.   Muundo huu unaweza ukaleta misuguano (paralysis and deadlocks in decision making) katika kufanya maamuzi juu ya masuala magumu ya kitaifa.

Rasimu imelitizama suala hili na kuliwekea masuluhisho yafuatayo;

(i)   Rasimu imeweka mifumo na vyombo vya kikatiba vya kuhakikisha hakuna misuguano na kwamba kuna fursa pana zaidi ya kufanya maamuzi kwa kuzingatia majadiliano, maridhiano na muafaka kwa maslahi ya Taifa na wananchi wa Tanzania. Rasimu inaanzisha Tume ya Uhusiano na Uratibu ambayo ndani yake ina viongozi wakuu ambao wana jukumu ya kulitizama taifa. Mwenyekiti wa Tume ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, wajumbe ni Rais wa Tanganyika, Rais wa Zanzibar, Mawaziri Wakaazi wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje. Utagundua kila mtu anayeweza kuamua yupo, rejea Ibara ya 109

(ii)  Kuna njia rasmi na zisizo rasmi za kutatua migogoro au kuondoa misuguano katika kufanya maamuzi na zimefafanuliwa bayana katika Rasimu Toleo la Pili. Njia rasmi ni pamoja na Tume ya Uhusiano na Uratibu, lakini pia iwapo majadiliano yatashindikana na ukatangazwa kuwa ni mgogoro basi mgogoro huwa utapelekwa kwenye Mahakama ya Juu ya Jamhuri ya Muungano ambayo uamuzi wake utakuwa ni wa mwisho, rejea Ibara za 111(1)(e), 111(2) na 156

(iii)Njia nyingine za kutatua migogoro na kuondoa misuguano katika kufanya maamuzi kama Tume imeshindwa ni pamoja na kumtumia Rais na Taasisi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano, rejea Ibara za 71 na 72

(iv)Njia nyingine ni pamoja na Baraza la Ulinzi na Usalama ambalo limepewa dhamana ya kuunganisha sera za ndani, kushughulikia masuala ya ulinzi na usalama, rejea ibara ya 237 na 238.

0 comments:

Post a Comment