Plus 255 Studios

Plus 255 Studios
Home » » Mshahara wa Rais kaa la moto

Mshahara wa Rais kaa la moto

Kwa ufupi
Waziri Kombani ang’aka, amvaa Zitto, wasomi, wanaharakati wasema wananchi wana haki kujua

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe kutaja hadharani mishahara ya Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, serikali imekataa kuizungumzia mishahara hiyo.
Msimamo wa Serikali kutotaja mishahara ya viongozi wakuu unatofautiana na utamaduni wa nchi nyingine kama Marekani, Afrika Kusini, Ufaransa na Kenya ambazo mishahara ya wakuu wake huwekwa wazi kwa umma.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema akiwa wilayani Igunga Mkoani Tabora, alisema Rais Kikwete anapokea zaidi ya Sh30 milioni kwa mwezi (sawa na Sh360 milioni kwa mwaka) ikiwa ni marupuru na mshahara kwa mwezi bila kodi, huku Pinda akipokea Sh 26 milioni kwa mwezi.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani alisema kiongozi yeyote haruhusiwi kutaja mshahara wa mtu mwingine kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria ya utumishi wa umma.
“Kuutaja mshahara wa mtu mwingine ni kinyume cha sheria na kosa, siyo utaratibu. Kwani wewe upo tayari watu waujue mshahara wako?” alihoji.
Aliongeza kuwa ingawa mishahara ya viongozi hao inatokana na kodi za wananchi, sheria ndiyo inayozuia watu kuyataja malipo hayo hadharani na kwamba hayupo tayari kuutaja mshahara wa rais au kiongozi mwingine labda mtu huyo autaje yeye mwenyewe.
“Siwezi kutaja mshahara wa bosi wangu wala wa kwangu mwenyewe. Wewe unaujua mshahara wa Obama (Rais wa Marekani)?” alihoji tena.
Akizungumzia mishahara ya marais wa nchi nyingine duniani kuwekwa wazi, Kombani alisema kila nchi ina utaratibu wake na kwamba Tanzania haijafikia hatua hiyo.
Alipotafutwa kulizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue simu yake ya mkononi iliita bila kupokewa. Gazeti hili pia liliwasiliana na Naibu Mtendaji Mkuu mwenye jukumu la kuanzisha na kuongoza Idara ya Mageuzi ya Kilimo Ofisi ya Rais Ikulu, Peniel Lyimo ambaye alisema yeye si mhusika. “Masuala yote yanayohusu utumishi yapo Wizara ya Utumishi,” alisema Lyimo.
Akianika mshahara wa Waziri Mkuu, Zitto alisema kwamba kiongozi huyo analipwa Sh11.2 milioni kama mbunge, Sh8 milioni kama waziri na Sh7 milioni kwa nafasi yake ya Waziri Mkuu, hivyo, kumfanya kupokea zaidi ya Sh300 milioni kwa mwaka.
Hata hivyo, Kombani alilionya gazeti hili kuandika taarifa za mishahara ya watu kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Bashiru Ally alisema Mwalimu Nyerere aliwahi kutaja mshahara wake hadharani na kuhoji viongozi wanaotaka mishahara yao isitajwe wanaficha nini.

0 comments:

Post a Comment