Ni baada ya kutoridhika na taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Dar es Salaam. Chama cha Wananchi
(CUF) kimesema kinakusudia kumwandikia Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano, Anne Makinda kikimwomba azielekeze kamati mbalimbali za Bunge
jinsi ya kufanya kazi zao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Katibu
Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema chama chake kimesikitishwa na
taarifa zilizotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe.
“Chama chetu kinatafakari hatua za kuchukua
ikiwemo kumwandikia Spika ili azifundishe kamati zake namna bora ya
kufanya kazi zake kama kamati za umma. Tumesikitishwa na kauli
tulizozisikia kupitia vyombo vya habari kuwa, chama chetu ni miongoni
mwa vyama kadhaa ambavyo havijawasilisha hesabu kwa Mkaguzi Mkuu wa
Serikali kwa kipindi cha miaka minne sasa. Tunaomba Watanzania wazipuuze
taarifa hizo kutuhusu kwa sababu hazina ukweli wowote,” alisema
Mtatiro.
Wiki iliyopita, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC), chini ya Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe alisema
licha ya kuwa vimepokea ruzuku ya jumla ya Sh67.7 bilioni kwa vyama tisa
vya siasa tangu mwaka 2009, vyama vyote vinavyopata ruzuku ya Serikali
havijawahi kupeleka ripoti yoyote ya ukaguzi wa fedha kwa CAG.
Kamati hiyo vilevile ilitangaza kusitishwa mara
moja utoaji wa ruzuku kwa vyama vyote vya siasa nchini mpaka hapo hesabu
zake zitakapokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).
Mtatiro alisema CUF kimesikitishwa na kufadhaishwa
na hatua ya kamati kuvihukumu vyama vyote vya siasa wakati jambo hili
ni la chama kimoja kimoja.
“Mbaya zaidi ni pale ambapo Mwenyekiti wa Kamati
ya PAC, Zitto amekuwa akishinda kwenye mitandao ya kijamii akishupalia
kuvichukulia hatua vyama – kikiwemo chama chetu, huku akiwa hana taarifa
za kina za namna tulivyotekeleza wajibu wetu,” alisema.
Alisema ni jambo la kufedhehesha kwa kamati ya
Bunge kushinda kwenye mitandao ya kijamii ikihukumu na kutoa taarifa za
uongo kwa umma bila hata kuwasiliana na vyama vya siasa na kumwomba
Spika azipe mwongozo kamati hizo.
THE ENQUISITOR
0 comments:
Post a Comment