Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, imewabeza watu, hususan
wanasiasa wanaosimama majukwaani kueleza Muundo wa Muungano wa Serikali
tatu utaongeza gharama za kiuendeshaji kuwa ni uongo na sababu hizo
hazina tija.
Mjumbe wa Tume hiyo, Humphrey Polepole alisema
hayo jana wakati wa mkutano wa kuijadili Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba
Mpya mbele wa Wajumbe wa Baraza la Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara.
Alisema Muundo wa Serikali tatu hauna gharama
zozote kwani chanzo cha mapato cha kuongoza Serikali ya Muungano kuwa
tayari kimebainishwa.
Polepole alisema gharama za kuongoza Serikali hiyo
zitatokana na Kodi ya Ushuru wa Bidhaa ambapo jumla yake zinazokusanywa
si chini ya Sh1 trilioni.
“Mpaka sasa Serikali ya Muungano inakusanya zaidi
ya Sh3 trilioni hivyo kama itatumika Sh1 trilioni na zitakazobaki
zitaelekezwa katika shuguli zingine, fedha zitakuwepo,” alisema Polepole
na kuongeza:
“Nashangaa wanasiasa wanaosimama majukwaani
kueleza wananchi kuwa kutakuwa na mzigo wa gharama, hii si kweli kwani
Tume tumekwisha bainisha chanzo chake cha mapato na hao wanaozungumza
hayo hawafuatilii mchakato kwa umakini.”
Alisema uchambuzi walioufanya juu ya kodi
inayokusanywa mwaka 2003/04 zilikusanywa jumla ya Sh500 bilioni na mwaka
2011/12 zilikusanywa Sh1 trilioni ambapo kila mwaka mapato hayo
yanaongezeka.
“Uzoefu unaonyesha kila mwaka mapato yanaongezeka
hivyo uwepo wa Muungano wa Serikali tatu ni dhahiri hautaathiri kitu
chochote na utasaidia kutatua kero zilizopo zinazojitokeza kila mwaka
kila kukicha,” alisema Polepole
Polepole aliwataka Wananchi kutokuwa na shaka na
mapendekezo hayo ya Tume juu ya Muundo wa Muungano kuwa wa Serikali tatu
kwani utapunguza malalamiko ya muda mrefu yaliyopo.
“Hivi sasa kuna kero zaidi ya 47 na kwa Muungano
huu uliopo hautamaliza na wala hauwezi kuyafanyia kazi lakini kutokana
na mapendekezo ya Tume ya Serikali tatu ninahakika yatapungua na kila
upande kutokuwa na malalamiko,” alisema Polepole.
Polepole amesisitiza kwa kuwaomba wananchi kuendelea kutoa maoni katika hali ya kutoshinikizwa kwa namna yoyote.
“Kila mtu anapaswa kuwa huru kutoa maoni yake bila
kuogopa chochote. Lengo la uwepo wa katiba mpya ni kujua hitaji hasa la
wananchi ni nini na kwamba katika kutoa maoni wananchi wanapaswa
kufanya hivyo bila woga,” alisisitiza Polepole.
0 comments:
Post a Comment