Dar es Salaam. Wasomi wameonyesha wasiwasi wao juu ya mazungumzo
kati ya Rais Jakaya Kikwete na vyama vya siasa vya upinzani vyenye
wabunge, kuhusu tofauti zilizojitokeza katika Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Wasomi hao licha ya kuunga mkono mazungumzo,
wamesema wanasiasa wana kawaida ya kuwa na agenda za siri jambo ambalo
baadaye huzusha tena mzozo, huku wakirejea kwamba si mara ya kwanza kwa
Rais Kikwete kufanya mkutano wa aina hiyo.
Kauli hizo zimetokana na Rais Kikwete kukutana na
viongozi wa vyama vya siasa; CCM, Chadema, CUF, NCCR Mageuzi, TLP na UDP
kukubaliana kuweka pembeni tofauti za kiitikadi na kutanguliza masilahi
ya taifa katika mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya.
Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam
(UDSM), Dk Azavery Lwaitama alisema uamuzi wa Rais Kikwete ni mzuri
lakini unaweza ukawa umechezwa kwa karata ya kisiasa.
Alifafanua, “Inaweza kuwa karata ya kisiasa kwa
sababu bado Bunge lina wabunge wengi wa CCM, pia marekebisho
yatasimamiwa na Waziri wa Katiba na Sheria, (Mathias Chikawe) sijui
kutakuwa na jipya gani.”
Lwaitama alisema ili mambo yaende sawa, Rais
Kikwete anatakiwa kuhakikisha kuwa marekebisho hayo yatakayofanywa nje
ya Bunge, hayabadilishwi tena bungeni. “Ahakikishe kuwa wabunge
wanapitisha tu yale ambayo yamerekebishwa nje ya Bunge.”
Naye Profesa Gaudence Mpangala wa UDSM alisema:
“Tutajua kama hili jambo limetulia ama la, kama Bunge likipitisha
mapendekezo mapya, kama ikiwa hivyo mambo yatakwenda vizuri.”
Hata hivyo, Profesa Mpangala alionyesha wasiwasi
wake kama wabunge wataamua kuyapinga mabadiliko hayo, huku akishauri
itumike njia ambayo itawafanya wabunge kukubaliana na kile
kilichojadiliwa nje ya Bunge.
Alisema Katiba nzuri ni lazima itokane na mwafaka wa pamoja na kwamba nia ya Rais Kikwete inapaswa kuendelezwa hadi bungeni.
Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Bashiru Ally
alisema: “Siku zote mtu asiyejua anapokwenda hawezi kupotea njia,
mchakato wa Katiba Mpya una mgongano wa mtazamo kuna maswali mengi
kuhusu mchakato huu kuwa wa kisiasa na kisheria.
Alisema kuwa mchakato huo sasa haujulikani
unaendeshwa kwa masilahi ya nani, kwa sababu kila malalamiko mengi
yanayotolewa yamebebwa na vyama vya siasa.
“Tupo njiapanda, binafsi sina imani kubwa na mchakato huu, vyama vimeweka masilahi yao zaidi mbele,” alisema Bashiru.
0 comments:
Post a Comment