Dar es Salaam. Siku chache baada ya Dk Kitila
Mkumbo kuvuliwa ujumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nao
umemsimamisha kuongoza Kitivo cha Elimu cha Chuo Kikuu Kishiriki cha
Elimu cha Dar es Salaam (Duce).
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Profesa Yunus Mgaya alisema Dk Kitila amesimamishwa kwa muda
usiojulikana baada ya uongozi kupata taarifa kwenye vyombo vya habari
kuwa ni kiongozi wa Chadema wakati akiwa mtumishi wa umma, jambo ambalo
ni kinyume cha sheria za nchi.
Profesa Mgaya alisema Dk Kitila alipewa barua ya
kusimamishwa Ijumaa iliyopita na sasa atabakia kuwa mhadhiri mwandamizi
kwenye kitivo hicho.
Alipoulizwa juu ya suala hilo, Dk Kitila alikiri kupokea barua ya kusimamishwa wadhifa wa Mkuu wa Kitivo cha Elimu.
“Ni kweli nimepokea barua ya kusimamishwa lakini kwa sasa siwezi kuzungumza zaidi,” alisema Dk Kitila.
Profesa Mgaya alisema UDSM kilikuwa kinafahamu
kuwa Dk Kitila alikuwa mwanachama wa kawaida wa Chadema na siyo
kiongozi. Alisema uongozi wa chuo hicho utaunda timu maalumu ya
kuchunguza suala hilo na itaanza kazi mara moja.
Profesa Mgaya alisema timu hiyo itakuwa na kazi
mbili, kwanza kuchunguza kama kweli Dk Kitila alikuwa Mjumbe wa Kamati
Kuu ya Chadema na kisha kupata maelezo ya Dk Kitila juu ya suala hilo.
Hivi karibuni, Dk Kitila na aliyekuwa Naibu Katibu
Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe walivuliwa nyadhifa zao zote ndani ya
chama hicho kwa madai ya kuandaa waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013
kinyume cha itifaki na sheria za chama hicho.
“Tumemsimamisha (Dk Kitila), ili kupisha
uchunguzi, tunataka tujiridhishe na yale yanayoandikwa na vyombo vya
habari, pia kumpa nafasi ya kujitetea, hatuwezi kumsimamisha tu na kukaa
kimya, tunataka kufanya mambo kisheria,” alisema Profesa Mgaya.
“Timu yetu itakwenda huko Chadema kupata taarifa
zaidi na Dk Mkumbo pia atasikilizwa,” alisema Profesa Mgaya na kuongeza
kuwa timu hiyo itafanya kazi yake ndani ya muda mfupi na matokeo ya
uchunguzi wake ndiyo yatakayoamua hatima yake.
Dk Kitila kusimamishwa Chadema
Kamati Kuu ya Chadema ilikutana Dar es Salaam
Novemba 20 na 21 na kuamua kuwavua uongozi, Dk Mkumbo, Zitto na
aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha Samson Mwigamba baada
ya kuwatuhumu kuhusika kuandaa waraka huo ambao ulilenga kuhamasisha
mabadiliko makubwa katika uongozi wa ngazi ya juu ya chama hicho katika
uchaguzi wake mkuu ambao umepangwa kufanyika Juni mwakani.
0 comments:
Post a Comment