Pwani. Mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwani
Kikwete ameibuka kidedea katika kinyang’anyiro cha kura za maoni za
kuwania ubunge katika Jimbo la Chalinze, Mkoa wa Pwani.
Katika uchaguzi huo, Ridhiwani aliongoza kwa
kupata kura 758 na kuwabwaga wenzake watatu, aliyekuwa Mwenyekiti wa
Yanga, Imani Madega aliyepata kura 335, Ramadhani Maneno (206) na
Changwa Mohamed Mkwazu aliyepata kura 17.
Katika uchaguzi huo, wapiga kura walitarajiwa kuwa 1,363 lakini waliojitokeza ni 1,321. Kura tano ziliharibika.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Saidi Bwanamdogo
kilichotokea Januari 22, mwaka huu.
Matokeo hayo yalitangazwa na Msimamizi Msaidizi wa
uchaguzi huo, Mjumbe Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Rugemalila
Rutatina katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Msata.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Ridhiwani
alisema ushindi alioupata si wa kwake binafsi, bali wa chama hicho
kinachoongozwa na Rais Kikwete.
Alisema baada ya kupatikana kwa mwakilishi wa
chama, makundi yote yanatakiwa kuvunjwa na kuunda moja la ushindi, kwa
kuwa kilichoongoza ni CCM na si Ridhiwani.
“Ndugu zangu nawashukuruni kwa ushindi mlionipa,
natambua walikuwapo marafiki zangu, ndugu zangu wa karibu wakiwanadi
wagombea wenzangu, lakini sasa nimepita mimi… nashauri kambi zetu
ziishie hapa uwanjani tukitoka hapa tuwe na lugha moja ya kukinadi chama
chetu,” alisema.
Kwa upande wake Madega alikiri uchaguzi huo kuwa na mchuano mkali kutokana na majina makubwa ya wagombea alioshindana nao.
Aliwataka viongozi wa chama wasiwabeze wagombea
walioshindwa, akisema wanastahili heshima zote ili kuwapa morali ya
kushirikiana kutetea jimbo hilo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika
Aprili 6, 2014.
Maneno alisema ni wajibu wa wanachama wa CCM
kuchagua kiongozi wanayemuona anafaa kupeperusha bendera, hivyo
iliwataka waliokuwa wanamuunga mkono kuelekeza nguvu zao kwa Ridhiwani.
0 comments:
Post a Comment