Plus 255 Studios

Plus 255 Studios
Home » » MASHARTI YA KATIBA YA ZANZIBAR YANAYOVUNJA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MASHARTI YA KATIBA YA ZANZIBAR YANAYOVUNJA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

 
HAPA NIMECHAMBUA BAADHI YA VIFUNGU VYA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO 1977(2005) NA KATIKA YA ZANZIBAR 1984(2010)

1.  Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 inatamka kwamba Zanzibar ni Nchi na inatamka mipaka ya eneo lake katika Ibara ya 1 inayosema Zanzibar ni Nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

Katika Ibara yake ya 2 inatamka Zanzibar ni miongoni mwa Nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Þ   Masharti haya ni kinyume na Katiba ya Muungano Ibara ya 1 inayotamka Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.

2.  Katiba ya Zanzibar katika Ibara ya 26 inatamka kwamba Rais wa Zanzibar ni Mkuu wa Nchi ya Zanzibar

Þ   Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika Ibara ya 33(2) inatamka Rais wa Jamhuri ya Muungano ndiye Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu

3.  Katiba ya Zanzibar katika Ibara ya 2A inatamka kwamba Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali, Rais aweza kuigawa Zanzibar katika Mikoa, Wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.

Þ   Masharti haya ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 2(2) ambayo inatamka Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais aweza kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge: Isipokuwa kwamba Rais atashauriana kwanza na Rais wa Zanzibar kabla ya kuigawa Tanzania Zanzibar katika Mikoa, Wilaya au maeneo mengineyo.

4.  Katiba ya Zanzibar katika Ibara ya 132 inatamka kwamba Hakuna Sheria yoyote itakayopitishwa na Bunge la Muungano ambayo itatumika Zanzibar mpaka Sheria hiyo iwe ni kwa ajili ya mambo ya Muungano tu na ipitishwe kulingana na maelekezo yaliyo chini ya vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Sheria kama hiyo lazima ipelekwe mbele ya Baraza la Wawakilishi na Waziri anayehusika. Ibara hii inaeleza zaidi, pale Sheria ndogo inapoundwa kwa mujibu wa uwezo uliowekwa chini ya kijifungu cha 132(1) na (2) itatumika tu pale itakapotimiza shuruti zote zilizowekwa kwa matumizi ya Sheria Mama kama ilivyoainishwa katika kifungu hiki

Þ   Masharti haya ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 64 ambayo inatamka kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano ndilo lenye mamlaka ya kutunga sheria kwa mambo ya Muungano (Bara na Zanzibar) na yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara

5.  Katiba ya Zanzibar katika Sura ya 3 juu ya Kinga ya Haki za Lazima, Wajibu na Uhuru wa Mtu Binafsi, inatamka katika Ibara ya 24(3) kwamba, Rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahkama Kuu (Zanzibar) katika shauri lililofunguliwa dhidi ya masharti ya Sura hii ya Katiba yatasikilizwa na Mahkama Kuu (Zanzibar) mbele ya Majaji watatu bila ya kumjumuisha Jaji aliyeamua shauri hilo mara ya kwanza. Majaji hao watatu watateuliwa na Jaji Mkuu na uamuzi wao utakuwa ni wa mwisho na hautokatiwa rufaa kwenye Mahkama ya Rufaa ya Tanzania.

Þ   Masharti haya ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 117(1) na (4) ambayo inatamka kwamba Mahakama ya Rufani ndiyo yenye Mamlaka ya juu ya kutoa haki nchini na uamuzi wake ni wa mwisho.
#source; hamphrey polepole 


0 comments:

Post a Comment