Dhamira
njema na safi ya kupata Katiba aliyokuwa nayo Rais Jakaya Kikwete
ilikuwa itupatie Katiba Mpya kwa watanzania katika Mwaka 2014. Dhamira
hii ilitafsirika katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo sote ni
mashahidi iliandaliwa kwa kuzingatia maslahi mapana ya makundi yote na
umma wa watanzania.
Msingi mkuu wakati wa kuandikwa kwa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilikuwa majadiliano yenye staha na
ustaarabu, maridhiano na zaidi muafaka miongoni mwa wadau na Taifa kwa
ujumla.
Sote tu mashuhuda, Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliyoundwa baada ya mchakato shirikishi na uliojikita katika
majadiliano, maridhiano na muafaka, ilifanya kazi zake kwa weledi
mkubwa, uzalendo wa hali ya juu na kwa kuweka maslahi ya Taifa mbele.
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba ilikusanya maoni ya wananchi na sote tu
mashahidi nchini kote. Maoni ya wananchi yalikusanywa katika sehemu za
wazi ambako wananchi walihamasishwa kutoa maoni yao kwa uhuru na uwazi.
Hata
awamu ya kwanza ilipokwisha na Rasimu ya awali kutolewa sote
tulithibitisha kwamba kwa hakika maoni ya wananchi yalipewa uzito
uliostahili katika Rasimu hiyo. Awamu ya pili, iliyohusisha Mabaraza ya
Katiba ya aina mbili, yale yaliyosimamiwa na Tume katika ngazi ya Wilaya
na Serikali za Mitaa, na yale yaliyojisimamia yenyewe na kuendeshwa na
Taasisi mbalimbali.
Ni kwa bahati mbaya Mabaraza ya Katiba
yaliyosimamiwa na Tume yalighubikwa na mashinikizo kutoka vyama vya
siasa na hasa Chama cha Mapinduzi. Kitendo hiki hakikuondoa ukweli
kwamba Mabaraza ya Katiba ya Taasisi zaidi ya 600 yalitoa maoni yao kwa
uhuru na yalikuwa na hadhi sawa nay ale yaliyosimamiwa na Tume.
Hata
baada ya awamu ya pili kukamili Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikuja na
Rasimu ya Katiba Mpya Toleo la Pili ambayo bado ilikuwa imeakisi maoni,
matakwa, matarajio na ndoto za watanzania wanaopenda kuona Taifa lao
linajizaa upya kwa kupata Katiba Mpya kweli kweli itakayojibu changamoto
zao.
TUMAINI LA WATANZANIA LINALOPOTEA
Nitarudia
kusoma sote tu mashahidi kwamba awamu wa tatu ya Mchakato wa Katiba
Mpya imegubikwa na misimamo na maslahi binafsi ya vyama vya siasa na
kusahau maoni ya wananchi yaliwasilishwa katika Bunge Maalumu la Katiba
kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
inalitaka Bunge Maalumu kujadili Rasimu ya Katiba Mpya na Maudhui yake
kama iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ni
bahati mbaya tena kwamba, Rasimu ya Katiba Mpya imewekwa kando na
mjadala wa katika Bunge Maalumu umejikita katika Mapendekezo ambayo
hayamo katika Rasimu. Hali hii inapoteza uhalali wa Bunge Maalumu la
Katiba, si tu kwakuwa linakwenda kinyume na Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba kifungu cha 25 lakini kwasababu linakwenda kinyume na Matakwa ya
wananchi ambayo kwa ujumla wao yako katika Rasimu ya Katiba Mpya
iliyowasilishwa na Tume.
Ni bahati mbaya kwamba baadhi ya
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba hasa kutoka kundi la walio wengi
wamejivika jukumu lililokuwa la Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakidai
kupokea maoni mbadala ya wananchi, kitendo hiki ni kinyume na Sheria na
ukiukwaji wa kiasi kikubwa wa haki ya wananchi ambao kwa ujumla wao
walitoa maoni yao kwa Tume ya Katiba.
Sote tumeshuhudia
maoni ya wananchi yaliyo wasilishwa katika Rasimu ya Katiba Mpya
yakitupiliwa mbali, na Bunge Maalumu hasa na kundi la walio wengi.
Kitendo cha kupuuza maoni ya wananchi hakivumiliki. Bunge Maalumu
limegubikwa na vijembe, matusi na kubeza wote wanaosimamia maoni ya
wananchi kama yalivyo katika Rasimu ya Katiba Mpya.
Kitendo
cha kupuuzwa, kubezwa, kutukanwa na kukiuka Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba kwa kutojadili Rasimu ya Katiba Mpya na kuleta katika Bunge
Maalumu Maoni yasiyokuwemo katika Rasimu, kimepelekea vyama vya Siasa
vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na DP kutoka nje ya Bunge Maalumu.
Uamuzi
huu hautorudi nyuma mpaka pale maoni ya wananchi yatakapojadiliwa
katika Bunge Maalumu, mpaka pale vikao vya bunge maalumu la Katiba
vitakapoendeshwa kwa kuzingatia majadiliano yenye staha na ustaarabu,
maridhiano na kujenga muafaka wa kitaifa.
KUUTAZAMA MCHAKATO WA KATIBA KWA MACHO YA UCHAGUZI WA 2015
Nchi
yetu inapaswa kuingia katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi
Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Mwaka 2015. Ndoto ya watanzania
ilikuwa kutumia Katiba Mpya katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.
Kitendo
cha vyama vya siasa kuweka masilahi binafsi katika Mchakato wa kupata
Katiba Mpya kama mtaji na maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015
hakiwatendei haki watanzania. Kitendo cha kuweka mbele masilahi ya vyama
hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka kesho na kupuuza ndoto za
watanzania za miaka 50 ijayo si kitendo cha kizalendo hata kidogo.
Wakati
huu wa kuandikwa kwa Katiba Mpya ni fursa kwa watanzania kulipanga
Taifa lao kuelekea miaka zaidi ya 50 ijayo na sio kukidhi haja na
maslahi ya kundi fulani la watu wachache wasio na mapenzi mema na Taifa
hili kutoka chama fulani cha siasa.
Bado hatujachelewa na kama
kuna dhamira ya dhati, kujadili Rasimu na Maudhui yake na kuiboresha na
si kuleta mambo mapya. Tukapata Katiba Mpya ambayo bado inaweza kutumika
kuendesha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015. Tukiweza kufanya hivyo historia
itatukumbuka kwamba tuliliweka Taifa Mbele na tukaweka historia duniani
kuwa ndio Taifa ambali limeweza kuandika Katiba katika amani na katika
muda mfupi.
MWAKA 2015 BILA KATIBA MPYA: ATHARI ZAKE
Kama
tutakwenda katika uchaguzi mkuu wa Mwakani bila Katiba Mpya
tutaliingiza Taifa katika “Constitutional crisis”. Katiba inayotumika
sasa, Katiba ya Mwaka 1977, ina mapungufu mengi na haiwezi kutupatia
uchaguzi ulio huru na wa haki. Hatuwezi kuendelea kufanya Marekebisho ya
Katiba wakati Msingi wa Mkuu wa Katiba yenyewe si imara na thabiti.
Tukienda
katika Uchaguzi Mkuu Mwakani bila Katiba Mpya tutakwenda tukiwa
tumegawika kama Taifa, hali hii si njema kwa wananchi ambao wametuamini
na kutupa dhamana ya kuwaletea muafaka wa kitaifa.
Hatuwezi
kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ambayo haijawekewa vyombo vya kikatiba
ambavyo vitahakikisha uhuru wa Tume unalindwa na haki kutendeka
Hatuwezi kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani wakati Matokeo ya Uchaguzi wa Rais hayawezi kuhojiwa Mahakamani
Hatuwezi kwenda katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani wakati mifumo ya uchaguzi haiko sawasawa
Hatuwezi kwenda katika uchaguzi mkuu Mwakani wakati hoja ya mgombea huru haijapatiwa majibu.
# source: Humphrey pole pole
Home »
» MCHAKATO WA KATIBA MPYA: NI ZAIDI YA ZAWADI KWA WATANZANIA
MCHAKATO WA KATIBA MPYA: NI ZAIDI YA ZAWADI KWA WATANZANIA
Posted by Unknown
Posted on 05:05
with No comments
0 comments:
Post a Comment