Ndege kubwa ya jeshi la Qatar ambayo inasemekana kutumika kutorosha
wanyamapori 152 wakiwa hai, ilipata vibali vyote vya kutumia anga la
Tanzania.
Pia ndege hiyo, aina ya C17 yenye namba za usajili MAA/MAB, iliomba
kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa shughuli za
kidiplomasia.
Hayo yalielezwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini hapa na
shahidi wa 26 upande wa mashtaka, Kanali Nathaniel Paulo Msemwa wa Jeshi
la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kitengo cha Operesheni na Mafunzo.
Miongoni mwa wanyamapori waliobebwa na ndege hiyo ni twiga wanne wenye
thamani ya Sh170.5 milioni waliosafirishwa kwenda Arabuni.
Akitoa ushahidi wake kwa kuongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali,
Evetha Mushi, Kanali Msemwa alisema Novemba 11, 2010 alipokea nyaraka
tatu zinazohusu vibali vya ndege hiyo kutumia anga la Tanzania.
Moja ya nyaraka hizo ni maombi yaliyopokelewa kwa fax na Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kutoka ubalozi wa Qatar uliopo
Sanaa, Mashariki ya Kati.
“Hiyo barua iliyokuwa na neno urgent (haraka) ilikuwa inaomba kibali kwa
ajili ya ndege hiyo na tayari ilikuwa imeridhiwa na kamishina wa Wizara
ya Mambo ya Nje,” alisema Kanali Msemwa.
Kibali hicho chenye namba MMJ/2145/0018/Nov10 kilichopokelewa mahakamani
kama kielelezo kinaonyesha ndege hiyo ingetua KIA Novemba 24, 2010 na
kuondoka kuelekea Qatar Novemba 26, mwaka huo. Kanali Msemwa alisema
vibali hivyo vilipelekwa kwao (JWTZ) kwa sababu ya usalama wa nchi na
usalama wa ndege yenyewe kwa vile ilikuwa ni ya kijeshi, ingawa ilikuwa
katika kazi ya kidiplomasia.
Alieleza kwamba wakati ndege hiyo ikiwa KIA, ilikuwa chini ya Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege (TAA) na jeshi liliwajibika tu wakati ndege hiyo
ikiwa katika anga la Tanzania.
Shahidi wa 27, Inspekta Filicheshi Mlabule kutoka Idara ya Upelezi ya
Polisi, alisema kabla ya upelelezi, mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori,
Paul Sarakikiya alisema upelelezi wa awali ulionyesha kuwa wanyama hao
walisafirishwa bila kibali.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment