Wanaoendelea kudai uraia pacha, ama hawajasoma Rasimu au wana lao jambo.
Salamu zangu kwenu wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba, naendelea kuwapa moyo kwamba kazi mnayoifanya ni yetu na ninyi
miongoni mwetu mmeonekana wenye sifa na vigezo vya kuitenda kazi hiyo
ipasavyo.
Simamieni masilahi ya umma na masilahi ya nchi
yetu kwanza. Kwa hakika, masilahi ya wananchi na nchi yakiwekwa vizuri,
maslahi yetu binafsi na ya makundi yetu, yatapatikana kwa kuzingatia
usawa, sifa, vigezo, uzalendo na uamuzi tukiwa sisi wananchi.
Leo nitazungumzia hoja inayovuma mjini juu ya
uraia pacha. Nilitembelea mji wa Dodoma nikagundua hata Kamati za Bunge
Maalumu zina kazi katika hili. Nianze kukiri kwamba katika hoja hii nina
masilahi. Nina ndugu, jamaa na marafiki ambao wameondoka hapa nchini
miaka nenda rudi na baadhi yao wameamua kuchukua uraia wa huko waliko
ughaibuni.
Zaidi ya wale ndugu, jamaa na marafiki ambao
wamehamia ughaibuni, nimepata bahati ya kuwa na ndugu wa damu, ambao ni
raia wa nchi nyingine na baadhi yao wako hapa nchi jirani katika Afrika
Mashariki.
Nianze na mtazamo wa kawaida kabisa, ndugu hawa,
jamaa na marafiki zangu na hasa nizungumzie wale walioacha kuwa raia wa
Tanzania kwa kile kigezo cha kuchukua uraia wa nchi nyingine
hakujawaondolea ukweli kwamba wao bado ni Watanzania kwa asili na
nasaba. Uhusiano, mawasiliano na uhalisia wa udugu, ujamaa na urafiki
wetu haujabadilika hata kidogo. Nimeshuhudia hata pale ambapo kuna shida
au furaha hapa nyumbani, ama wameshiriki moja kwa moja au kwa michango
yao ya hali na mali.
Ni ukweli ulio dhahiri kabisa kwamba, hawakufanya
uamuzi wa kulazimishwa bali kwa namna moja au nyingine mazingira
yaliwafanya wajitafakari kubaki na uraia wa Tanzania na kukubali kubaki
na changamoto fulani wakiwa ughaibuni au wachukue uraia wa huko waliko,
ili kuweka wepesi wa hali lakini pia kupanua wigo wa fursa wanazoweza
kupata huko waliko kama raia.
Tafsiri ya uraia kwa ufupi
Kitabu cha taarifa na chenye kumbukumbu
(Insaiklopidia) cha Chuo Kikuu cha Stanford, kinatafsiri uraia
(citizenship) kama uanachama katika jamii ya kisiasa na unaonufaika na
haki, pamoja kuwa na wajibu katika uanachama huo. Dhana ya uraia
inajumuisha mambo matatu.
Moja, kwamba uraia ni hadhi ya kisheria
inayotafsirika kwa haki za kiraia, kisiasa na kijamii. Hapa, raia ni mtu
anayekwenda kwa mujibu wa sheria na ana haki ya kupata ulinzi wa
kisheria.
Mbili, ni raia kama mawakala wa kisiasa wanaoshiriki kikamilifu katika taasisi za kijamii na kisiasa.
Tatu, ni raia kama wanachama wa jamii ya kisiasa
inayoakisi aina fulani ya utambulisho. Utambulisho katika dhana ya uraia
ni jambo muhimu sana. Utambulisho huakisi uhusiano alionao mtu au raia
moja kwa moja ama kiasili au kinasaba na jamii fulani ya kisiasa.
Ikumbukwe katika suala la uraia, nchi (State), inatafsiriwa kama
Mamlaka Kuu (Sovereign Authority), yenye mamlaka kamili ya kutawala
watu katika eneo lake linalotambulika. Kama ilivyo mipaka ya kisheria ya
nchi inayoonyesha ukomo wa eneo lake, ndivyo dhana ya uraia
(citizenship) inavyoonyesha na kutambulisha watu walio chini ya Mamlaka
ya nchi fulani.
Leo hii nchi siyo tu ni nguvu za dola na taasisi
zake mbalimbali, bali pia ni jumuia ya wananchi kama wanachama. Uraia
kwa maana hiyo, ndiyo uanachama katika nchi. Kama ilivyo katika vilabu
vya mpira wa miguu, mfano Yanga au Simba, mtu unaweza kuwa mwanachama wa
Yanga au Simba, lakini siyo vilabu vyote viwili kwa pamoja.
Ubaya wa uraia pacha
Uraia pacha unaondoa ile dhana ya uaminifu
usiogawika (indivisible loyalty) kwa nchi na Mamlaka Kuu ya nchi. Kama
ambavyo mtu hawezi kutumikia wakuu wawili kwa wakati mmoja, vivyo hivyo
mtu hawezi kutumikia (kwa maana ya uaminifu na utii) nchi zaidi ya moja.
Uraia pacha unadhoofisha usalama wa taifa. Nieleze kwa mifano tu, miezi
kadhaa iliyopita kulitokea uvumi kwamba ofisa wetu wa Jeshi la
Wananchi, tena mwenye dhamana ya kutunza au kushughulika na taarifa
nyeti za kimawasiliano ametoweka.
Sote tu mashahidi kihoro tulichokipata kipindi
kile na zaidi uvumi ulipozidi kuwa huenda amekimbilia nchi fulani ya
jirani. Tukiwa na uraia pacha, hofu hii itaongezeka maradufu, hasa pale
wenye uraia pacha watakapopewa dhamana ya madaraka makubwa na nyeti.
Kuna mifano ya jamaa zetu, ambao tuliwafahamu kama
Watanzania, tukawasomesha kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania,
wakahitimu na tukawapa dhamana na madaraka makubwa na nyeti. Leo hii
angalau wale ambao mimi nawajua hawako nasi tena. Wamekwenda kwenye ile
nchi ambayo ni kama ilizaliwa upya na inasemekana inapiga hatua kubwa
kimaendeleo.
Kama uraia pacha ukiwapo, itakuwa vigumu kusema
hii ni siri na ni kwa masilahi ya taifa tena huenda dhidi ya mataifa
jirani kwa sababu hao wenzetu ambao pia watakuwa raia wa nchi jirani
tutakuwa nao tukitengeneza mambo hayo.
Tuchukue mfano mwingine, sasa tuna sera ya
kuhudumu katika jeshi kisheria kwa vijana wetu kama sehemu ya kujenga
ushupavu na kuimarisha uzalendo wao, tukiwa na uraia pacha tujiandae
kuwa na Warundi, Wakongo, Wamarekani, Wakenya na Wasomali JKT
tukiwafundisha uaminifu, utii na namna ya kuipenda Tanzania kwa moyo
wote hata na ikibidi mpaka tone la mwisho la damu yao.
Zaidi ya yote, uraia pacha unavunja msingi wa haki
ya usawa kwa sababu katika taifa moja, raia wanawekwa katika mafungu,
wale wenye uraia wa zaidi ya nchi moja, ambao wanakuwa na haki zote
nchini na haki zaidi kwingineko dhidi ya wale wenye uraia mmoja, ambao
wana haki zote za hapa nchini pekee, lakini wote wako sawa nchini.
Suluhisho ndani ya Rasimu ya Katiba Toleo la Pili
Rasimu inapendekeza bila kupepesa macho kwamba
uraia wa Jamhuri ya Muungano ni mmoja na utapatikana kwa njia mbili
kuzaliwa na kuandikishwa.
Ibara ya 59 ya Rasimu ya Katiba na kama
inavyofafanuliwa na Randama, inawatambua na kuwapa hadhi maalumu watu
wenye asili au nasaba ya Tanzania na ambao wameacha kuwa raia wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa kupata uraia wa nchi nyingine wanapokuja
Tanzania kwa masharti yatakayoainishwa na sheria za nchi.
Lengo la Ibara hii ni kuwapa hadhi maalumu watu walioacha kuwa
raia wa Jamhuri ya Muungano, tofauti na raia wa nchi nyingine ambao
hawana asili au nasaba ya Tanzania.
Sababu ya mapendekezo haya ni kuwawezesha watu
waliokuwa raia wa Tanzania waliopoteza uraia kwa namna yoyote ile kuwa
na hadhi maalumu wanapokuwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hadhi hiyo itawaondolea usumbufu wanaporejea Tanzania na kuwapa fursa
mbalimbali za kushiriki katika maendeleo ya nchi, jamii na familia zao
zilizobaki Tanzania.
Mapendekezo haya yalizingatia kuwa nchi
itakapotambua uraia wa nchi mbili, haitakuwa na msingi wa kikatiba na
kisheria wa kuwazuia raia wa nchi nyingine kubaki na uraia wao
wanapokuwa raia wa kuandikishwa wa Tanzania kwa kuzingatia kuwa Jamhuri
ya Muungano inapakana na nchi nane na italeta changamoto ya usalama na
ulinzi.
Uzoefu wa nchi nyingine
Uzoefu wa nchi ya India na Ethiopia ambazo hazina
na zimesita kutoa uraia wa nchi mbili kwa sababu za kiulinzi na usalama,
lakini zimetoa hadhi maalumu kwa watu wenye asili na nasaba ya nchi
hizo, ambao wameacha kuwa raia wa nchi hizo.
Katika Katiba ya India, watu hao wanaitwa ‘Persons
of Indian Origin’ na wana hadhi maalumu. Kwa mujibu wa sheria za India,
mtu mwenye asili au nasaba ya India hadi kizazi cha nne, atapata hadhi
ya ‘Person of Indian Origin (PIO)’, isipokuwa kwa raia wa nchi za
Afghanistan, Bangladesh, Bhutan, China, Iran, Nepal, Pakistan na
Sri-Lanka.
Watu wenye hadhi ya PIO wanaweza kupata fursa
zifuatazo: Kupata kadi ya kitambulisho cha PIO. Hahitaji viza ya kuingia
na kutoka India. Anaweza kukaa miezi sita nchini India mfululizo bila
kulazimika kujiandikisha uhamiaji. Wana haki sawa ya kupata huduma za
kiuchumi, kifedha na elimu kama ilivyo kwa raia wengine.
Wana haki ya kununua, kumiliki, kuhamisha, kuuza
mali isiyohamishika isipokuwa kwa mashamba makubwa ya kilimo. Watoto wao
wana haki ya kudahiliwa katika vyuo vya elimu ya juu nchini India. Wana
haki ya kupata makazi katika utaratibu unaosimamiwa na Serikali au
wakala wake.
Hata hivyo, watu wenye hadhi ya PIO hawana haki
zifuatazo: Hawaruhusiwi kupiga kura na hawaruhusiwi kugombea nafasi
yoyote ya kisiasa wala kushika madaraka ya utawala.
Wito wangu kwa wajumbe wa BMK na wananchi wenzangu
Tuisome Rasimu ya Katiba Mpya Toleo la Pili kwa
jicho chanya, tuyaelewe maudhui yake, tuone ni namna gani yanalenga
kuimarisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tulifuatilie Bunge Maalumu
kwa ukaribu na tuendelee kujadiliana kwa uwazi kwa maana ya kujenga.
Nchi yetu bado ni changa sana kuanza kuugawa uaminifu (loyalty) na utii
(allegiance) wetu kwake.
Tutaendelea Wiki Ijayo.
source: Mwananchi
source: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment