Mfumo wetu wa Sheria umejengwa kushughulikia mashauri ya kimila
na Kiislamu. Kwa unyenyekevu mkubwa, nikiri kwanza kwamba, mjadala huu
unaweza kufanikiwa iwapo tutaweka mbele kujifunza na kutafuta maarifa
kama ambavyo imani zote zinavyohubiri.
Tujadiliane kwa hoja na sababu huku mioyoni mwetu
tukiwa na uelewa wa pamoja wa misingi inayotuleta pamoja kama Taifa,
tukikusudia kujenga mwafaka na kufanya maridhiano. Tukiendelea na ile
dhambi ya watakacho wengi dhidi ya wachache bila hoja na sababu kwa
hakika itatutafuna na baadhi yetu tutasimama ili kuhukumiwa kiimani,
kisheria na kihistoria leo na katika vizazi vijavyo.
Utangulizi
Suala la Mahakama ya Kadhi limekuwa mojawapo ya
hoja muhimu sana hapa Tanzania, mjadala wake umechukua zaidi ya muongo
mmoja. Ili kulielewa suala hili ni muhimu kujifunza kwa kiasi mfumo wa
utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano na kisha kwa kiasi kuelewa ni
wakati gani na kwa mazingira gani Mahakama za Kadhi huwepo. Sambamba na
kuelewa mfumo wa utoaji haki ni vema pia kuelewa matumizi ya Sheria za
Kiislamu au “Sharia law” kwa ujumla wake au kwa sehemu.
“Sharia Law” kwa ujumla wake ni pana sana na
inajumuisha vitu vingi, uzoefu unaonyesha maeneo tofauti tofauti katika
ngazi ya nchi wanatumia Sharia Law kulingana na mazingira pamoja na
mahitaji ya eneo na jamii husika. Matumizi ya Sharia Law kwa namna moja
au nyingine yanategemeana sana na asili na historia ya eneo au jamii
husika, eneo au jamii yenye Waislamu wengi kuliko waumini wa dini
nyingine inawezekana Sheria Law ikatumika kwa ujumla wake. Maeneo ambayo
idadi ya waumini wa dini ya Kiislamu inakaribia kulingana na waumini wa
dini nyingine matumizi ya Sharia Law ni tofauti, na mara nyingi Sharia
Law huwa inatumika kwa sehemu na hasa katika kutoa uamuzi katika
mashauri yahusuyo ndoa, mirathi, talaka na wakf. Hata hivyo yako
mazingira ambayo eneo au jamii fulani inaweza kuwa na waislamu wachache
na Sheria Law ikatumika kwa sehemu. Mahakama ya Kadhi huwa ni chombo
kinachopewa dhamana ya kutoa maamuzi juu ya mashauri yanayohusu waumini
wa dini ya Kiislamu. Uhitaji wake, uanzishwaji, muundo na mfumo wake wa
kiutendaji hutegemea mazingira ya jamii husika. Mazingira haya
hutofautiana kutoka eneo moja hadi lingine lakini msingi huwa ni
historia, mfumo wa kisheria na idadi ya watu na uwiano wa waumini wa
dini ya Kiislamu na dini nyingine.
Uwepo wa Mahakama za Kadhi pale ambapo Waislamu ni
wengi kuliko waumini wa dini nyingine namna ya uanzishwaji wake pamoja
na muundo wake huwa ni tofauti na katika mazingira ambayo Waislamu wana
idadi sawa na waumini wengine na vivyo hivyo pale ambapo Waislamu ni
wachache katika jamii husika. Nitatumia mifano mitatu ya maeneo ambayo
kuna matumizi ya Sheria Law (matumizi ya jumla au kwa sehemu) pamoja na
uwepo wa Mahakama za Kadhi.
Mfumo wa utoaji haki Tanzania Bara
Kama nilivyoeleza hapo awali uwepo au kutokuwepo
Mahakama ya Kadhi kimuundo na kiutendaji ndani kikatiba na katika sheria
za nchi inategemea na mfumo wa kisheria au legal system katika eneo
husika. Mfumo wa kisheria huwa unataarifiwa na historia, desturi,
utamaduni na uhalisia.
Kwa hapa Tanzania mfumo wa sheria unataarifiwa na
vyanzo kadhaa vya sheria au kwa Kiingereza huitwa “sources of law”.
Sheria ya Judicature and Application of Laws Act CAP 358 inatamka bayana
kwamba vyanzo vya sheria ni pamoja na Sheria za Kurithi (baadhi ya
sheria za Uingereza), Sheria za Kimila (Customary Laws), Sheria za
Kiislamu (Islamic Laws), Statutory Laws (Sheria zinazotungwa na Bunge),
Case Laws (Maamuzi yanayofanywa na Mahakama), Baadhi ya Sheria za
Kihindi (Indian Acts) pamoja na Katiba ambayo ndiyo sheria mama.
Kwa maelezo tajwa hapo juu utagundua, mfumo wa
sheria wa Tanzania Bara unajumuisha matumizi ya Sheria za Kiislamu
katika muundo wake wa kimahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo. Kifungu cha
11(1)(ii) kinaweka bayana masuala ambayo kidesturi katika maeneo
mengine yangekuwa chini ya Mahakama ya Kadhi kwamba yanaweza kuamuliwa
na mfumo wetu wa kimahakama, kama kinavyojieleza “nothing in this
subsection shall preclude any court from applying the rules of Islamic
law in matters of marriage, divorce, guardianship, inheritance, wakf and
similar matters in relation to members of a community which follows
that law”. Kifungu hiki kinamaanisha “Mahakama yoyote haitazuiwa kutumia
kanuni za Sheria ya Kiislamu katika masuala ya ndoa, talaka, malezi,
urithi, wakf na masuala yahusianayo kwa waumini wa dini ya Kiislamu”,
tafsiri ni yangu.
Katika kuonyesha kwamba mfumo wetu wa kisheria
tangu awali umekuwa na dhamira ya kuona masuala ya Waislamu na watu
wafuatao mila (customs) yanafanyiwa maamuzi na mifumo na taasisi zetu
zenye dhamana ya kutoa haki nchini utagundua hata Sheria ya Magistrate
and Courts Act CAP 11 katika kifungu chake cha 7(3) inasema; “In any
proceeding in any other magistrates’ court in which any rule of
customary or Islamic law is in issue or relevant the court may, and when
directed by an appropriate judicial authority shall, sit with an
assessor or assessors; and every such assessor shall be required, before
judgment, to give his opinion as to all questions relating to customary
or Islamic law in issue in, or relevant to, the proceeding; save that
in determining the proceeding the court shall not be bound to conform
with the opinion of the assessors”.
Sheria hii inaendelea kutoa mamlaka kwa mfumo wetu
wa kimahakama kutoa uamuzi juu ya Mashauri yanayohusu waumini wa dini
ya kiislamu na hata wasio waislamu kisheria. Sheria inaweka bayana
kwamba wakati shauri la kimila au kiislamu linapoletwa katika mahakama
za mwanzo, hakimu atakaa na washauri ambao wataipa ushauri mahakama
katika suala husika. Washauri hawa wanapaswa wawe wamebobea katika eneo
husika. Sheria inakwenda mbali zaidi kuweka vigezo vya aina ya washauri
na namna ya kupatikana kwao ikiwemo hata marupurupu yao, rejea kifungu
cha 9 cha Sheria (MCA CAP 11).
Aina za utolewaji haki kwa masuala ya Kiislamu
Suala la utolewaji haki katika mashauri ya
Kiislamu hasa yale yahusuyo ndoa, talaka, malezi, urithi, wakf na
masuala yahusianayo kwa waumini wa dini ya Kiislamu ni masuala ya
kitaaluma, ni masuala ya elimu, “ilmu” au kwa Kiingereza ningesema ni
jurisprudential na kwa kiasi fulani tofauti na imani na dini nyingine.
Nifafanue aina mbili za Mahakama za Kadhi na kama ambavyo zilivyo
Zanzibar na katika nchi mbalimbali ikiwemo Kenya, Uganda, Nigeria, India
n.k.
Ziko Mahakama za Kadhi zenye mrengo wa Ibada au
kwa lugha nyingine “Ibadat”, Mahakama hizi na utendaji wa shughuli zake
husimamiwa na taasisi za kidini na ni sehemu ya ibada. Mfano wa Mahakama
za Kadhi zenye mrengo wa “Ibadat” ni katika baadhi ya majimbo ya
kaskazini kule nchini Nigeria.
Mara nyingi hutumia sharia law kwa ujumla wake.
Wenye dhamana ya kuamua mashauri katika mahakama hizi huwa ni viongozi
wa kiimani wenye uelewa na sharia law. Mahakama zenye mrengo wa ibadat
huwa huru “independent” na maamuzi yake huwa ya mwisho na kikatiba huwa
si sehemu ya Mamlaka ya Dola hasa pale inapokuwa dola linaundwa na
waumini wa dini mbalimbali.
Uko utaratibu wa kutoa haki kwa masuala ya
Kiislamu kwa misingi ya elimu ya dini au kwa lugha nyingine “Muamalat”,
utaratibu huu umejikita katika taaluma ya sheria za Kiislamu kwa maana
ya matumizi, maamuzi na watoa maamuzi kwa maneno mengine misingi yake
imejengwa zaidi katika uelewa na maarifa ya taaluma ya sheria au
jurisprudence. Wanaotoa maamuzi si lazima wawe viongozi wa kiimani pekee
bali wale waliobobea katika sheria za Kiislamu au Islamic law.
Utolewaji haki kwa mashauri ya Kiislamu katika msingi wa Muamalat katika
maeneo na nchi tofauti tofauti na kulingana na historia, mapokeo,
uhalisia wa mfumo wa kisheria pamoja na mtangamano wa watu kutoka dini
mbalimbali zinachukua sura kadhaa wa kadhaa, moja, msingi mkuu si ibada
bali taaluma ya sheria, pili, katika baadhi ya maeneo utaratibu huu ni
sehemu ya mfumo wa kisheria na kitaasisi na sehemu ya Mamlaka, mfano
mzuri ni Zanzibar. Tatu, katika maeneo mengine na nchi kadhaa utolewaji
haki kwa masuala ya Kiislamu ni sehemu ya mfumo wa sheria unaoelekeza
namna ya utolewaji haki katika mashauri ya Kiislamu na mfano mzuri ni
katika baadhi ya majimbo ya kusini mwa Nigeria na hapa Tanzania Bara,
kabla na baada ya uhuru.
Mfano wa hakimu (mwajiriwa wa Serikali) aliyefanya
kazi kabla ya uhuru akitoa hukumu kwa mashauri ya Kiislamu wa weledi
mkubwa ni Mathiasi Mnyapala aliyekuwa Liwali hapa Dar es Salaam. Miaka
ya themanini Mwishoni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilipeleka wanafunzi
wawili kwenda kusomea shahada ya uzamili katika Sheria za Kiislamu
katika Chuo Kikuu cha London SOAS ambao leo hii ni Jaji Profesa Ibrahim
Juma, Jaji wa Mahakama ya Rufaa na Jaji wa Mahakama Kuu Robert
Makaramba, Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Biashara. Tujifunze kwa
wanataaluma hawa.
Je, ni Ibadat au Muamalat?
Hitaji la Mahakama ya Kadhi linapaswa kuenda
sambamba na swali la ni Je, ni utaratibu upi wa kutoa haki kwa mashauri
ya Kiislamu, ni “Ibadat” au “Muamalat”? Kama jibu ni Ibadat basi waumini
wa dini ya Kiislamu wanapaswa kutoa uongozi katika hili, ibada ni suala
la imani na ni budi kwa waumini kulifanyia kazi ili Mahakama
zilizoanzishwa zikidhi hitaji. Sheria ya Ndoa au Law of Marriage Act CAP
29 ni mfano mdogo wa kuanza kutambua nafasi ya Kadhi katika ndoa kama
sehemu ya Ibada.
Kama jibu ni Muamalat basi jibu ni kwamba Mfumo wa
Kisheria wa Tanzania Bara tayari umejumuisha kama chanzo cha Sheria
zake, Sheria za Kiislamu au Islamic Law. Kinachotakiwa kufanyika ni
kufanyia kazi maelekezo ya Sheria ya The Islamic law (Restatement) Act
CAP 375 katika kifungu chake cha 2 na 3. Nimefuatilia jambo hili na
ninashauri waumini wa dini ya Kiislamu wakae na waziri wa Sheria
walimalize hili ili Mahakama zetu ziweze kutoa hukumu kwa mashauri ya
Kiislamu zikiwa na mwongozo sahihi.
Itaendelea wiki ijayo
0 comments:
Post a Comment