Dar es Salaam. Wenyeviti wenza wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jana waliuteka Mkutano Mkuu wa Chadema kwa hotuba zilizotoa msimamo wa umoja huo katika mchakato wa Katiba mpya.
Huku wakishangiliwa na wanachama zaidi ya 900 wa
Chadema, wenyeviti hao Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia
(NCCR-Mageuzi) na Dk Emmanuel Makaidi (NLD) walisema umoja wao
hautaishia kudai Katiba mpya iliyotokana na maoni ya wananchi, bali
utaendelea hadi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Ukawa inaundwa na vyama vya Chadema, CUF, DP, NLD na NCCR-Mageuzi.
Viongozi wengine waliozungumza katika mkutano huo
ni makamu mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula na msajili wa Vyama vya
Siasa, Jaji Francis Mutungi.
Wakati wa utambulisho, katibu mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa aliwataja viongozi hao kuwa ni marafiki wa damu huku
akimtambulisha Mangula kuwa ni rafiki na mtani wa jadi.
Mbatia
Huku akishangiliwa kila alipotamka neno “people’s
power”, Mbatia alianza kwa kuwahoji wanachama wa Chadema, “serikali
ngapi?” na kujibiwa “tatu”.
Alisema mkutano huo ni ishara ya Tanzania kuandika
historia mpya, hivyo ni lazima iongozwe na viongozi makini huku
akiwataka wanachama wa Chadema kutofanya makosa kwa kuchagua viongozi
ambao si makini.
“Miaka ya nyuma tulifanya makosa na tuliteleza,
ila tukumbuke kuwa makosa ya zamani ni mafundisho yetu ya mbele.
Kiongozi mzuri ana sifa tano ambazo ni uwezo wa kupanga hoja,
ushirikiano, kuratibu, kutoa maelekezo na kusimamia. Sifa hizo tano
Mbowe anazo,” alisema na kushangiliwa kwa nguvu.
Alisema hatua iliyofikia Ukawa ni nzuri, hivyo
viongozi wa vyama vinavyounda umoja huo wanatakiwa kuwa makini,
kuheshimiana na kuaminiana ili kufikia malengo waliyojiwekea.
“Tanzania ni yetu sote, si ya CCM peke yao na hilo Mangula analijua,” alisema.
Alisema katika mkutano kati ya Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD) na Rais Jakaya Kikwete walikubaliana kuwa
mchakato wa Katiba mpya usitishwe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka
2015.
“Tulikubaliana kufanya marekebisho katika sheria na Katiba ya
sasa kuhusu tume huru ya uchaguzi, matokeo ya Rais kuhojiwa mahakamani,
kuruhusu mgombea binafsi na mshindi atangazwe baada ya kuchaguliwa kwa
zaidi ya asilimia 50 ya waliopiga kura.
“Pia tumekubaliana kuwa msingi wa Rasimu ya Katiba
uheshimiwe. Pamoja na hayo Bunge la Katiba bado linaendelea, huu ni
sawa na ufisadi. Uamuzi kuhusu mchakato wa Katiba utakaotolewa katika
mkutano huu tutauheshimu?”
Mbatia alisema Chadema ni chama kikuu cha upinzani
Tanzania Bara kama ilivyo kwa CUF Zanzibar, hivyo akavitaka vyama hivyo
kukaa meza moja na CCM kuzungumza na kukubaliana kwa masilahi ya
Watanzania, “Msionyeshane ubabe baina yenu. Hatuwezi kukubali watu
wahuni waharibu Taifa letu.”
Profesa Lipumba
Huku akitumia maneno ya utani na mafumbo, Profesa
Lipumba alisema: “Kuelekea katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 tutakuwa na
wimbo wetu wa pamoja ambao ni ‘bye bye CCM’.”
Alisema kukwama kwa mchakato wa Katiba kunatokana
na wazo la kuandika Katiba mpya lililotolewa na Rais Kikwete kutokuwamo
katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
“Rasimu ya Katiba ina misingi ya uwajibikaji na
wenzetu (CCM) kwa kulitambua hilo wameamua kuinyonga na kuweka mambo yao
kwa ajili ya ulaji,” alisema. Alilaani kitendo cha Bunge la Katiba
kuendelea na vikao vyake wakati tayari Ukawa kupitia TCD
wameshakubaliana na Rais kuwa viahirishwe.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2015, Profesa Lipumba
alisema: “Sasa ni muhimu vyama vinavyounda Ukawa vifanye mkutano mkuu wa
kupendekeza nani atakuwa mgombea urais.”
Dk Makaidi
Alisema, “Ukawa ni tumaini la Watanzania. Kama ni kuogelea tutaogelea pamoja na ikiwa ni kuzama basi tutazama pamoja.”
Huku akizungumza kwa msisitizo na ushawishi, Dk
Makaidi alisema Watanzania wanasubiri kwa hamu maazimio ya Chadema
katika mkutano huo, huku akikitaka chama hicho kuhakikisha kinatoa
maazimio ya maana. “... suala la Katiba mpya lipo njiapanda na hatujui
huko mbele tutakwenda vipi. Tunataka kusikia maazimio yatakayoleta
matumaini kwa Watanzania,” alisema.
Mangula
Kwa upande wake, Mangula aliyemwakilisha
mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete alisema siasa siyo chuki wala ugomvi,
bali ni tofauti za kisera, kiitikadi na kifalsafa na kusisitiza kuwa
utaratibu wa vyama vya siasa kukutana mara kwa mara utawaweka karibu
zaidi.
Alisema: “Tunapokutana tunajenga utaratibu wa
kuvumiliana kisiasa na tuweke nchi mbele na vyama baadaye. Siasa ni
kukubali kupokea mawazo tofauti ya mwenzako.”
alisema. na hata mimi (Mangula) nakubali hilo,” alisema.
Alisema tofauti za kisiasa zisiwe chanzo cha
viongozi kujenga chuki, “Tuwe kama mashabiki wa Simba na Yanga ambao
wanakuwa na upinzani uwanjani, lakini mchezo ukimalizika kila mtu
anaendelea na shughuli zake.”
Alisema amejifunza kitu katika mkutano huo akisema
ni hamasa, wingi wa watu na jinsi chama hicho kinavyopeleka demokrasia
mbele tofauti na mikutano mingine ya awali ya vyama vingine.
Jaji Mutungi
Katika hotuba yake fupi, Jaji Mutungi ambaye
alishangiliwa kwa nguvu kutokana na kauli yake ya hivi karibuni kuhusu
kutotambua mabadiliko ya Katiba ya Chadema, alisisitiza umuhimu wa
demokrasia ndani ya vyama vya siasa na kuvitaka vizingatie amani.
“Utulivu ambao mmeuonyesha leo katika uchaguzi huu uendelee kuwa hivi hata baada ya kumalizika na hata katika ngazi za chini.”
Sheikh atoa mpya
Alipopewa nafasi ya kuomba dua kabla ya kuanza kwa
mkutano huo, Sheikh Rajabu Katimba wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu
Tanzania, pamoja na dua hiyo, alisema sasa umefikia wakati wa kuiondoa
CCM madarakani kwa maelezo kuwa tangu nchi ipate uhuru chama hicho
kimeshindwa kuiletea nchi maendeleo.
0 comments:
Post a Comment