RASIMU YA KATIBA TOLEO LA PILI ILISHATOA MAJIBU KWA CHANGAMOTO ZOTE ZA SERIKALI 3
NINAANDIKA KAMA SEHEMU YA KUONDOA HOFU KWA WALE WENYE HOFU
Hofu iliyozungumzwa juu ya Serikali 3 haina mashiko na ni ya kufikirika zaidi
Leo
nimeona nifafanue hii sintofahamu kuhusu changamoto za Muundo wa
Serikali Tatu. Kimsingi muundo huu ukiacha ukweli kwamba wananchi
wameutolea maoni, kwa hoja na sababu lakini pia Tume ya Katiba
iliufanyia utafiti, ikazingatia uhalisia wa historia na uhalisia wa
utendaji katika mazingira ya sasa. Kwa unyenyekevu mkubwa nieleze
changamoto zilizoibuliwa na Taarifa ya Utafiti juu ya Masuala ya
Muungano na nieleze majibu ambayo Rasimu imeyatoa kwa umakini mkubwa.
Majibu ninayoyatoa hapa yametolewa pia katika Ripoti ya Tume juu ya
Mchakato wa Katiba Mpya. Nitoe rai watu kuzungumza changamoto za muundo
huu na kuona ni mapendekezo gani yametolewa kukabiliana na changamoto
hizo. Naomba usomapo Makala hii fanya rejea kwenye Rasimu ya Katiba
Toleo la Pili.
Changamoto hizo ni kama ifuatavyo;
1. Muundo huu unaweza ukawa na gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma;
Muundo unaopendekezwa katika Rasimu hauna gharama kwasababu zifuatazo kwa ufupi;
(i) Mambo ya Muungano ni Machache, yamepungua kutoka 22 hadi 7, Ibara ya 63
(ii) Mambo ya yasiyo ya Muungano sasa yatatekelezwa na Tanganyika na Zanzibar Ibara ya 64
(iii)Serikali ya Jamhuri ya Muungano ni ina Mamlaka Makubwa ila ndogo, Mawaziri wake hawatozidi 15, Ibara ya 98
(iv)Bunge la Jamhuri ya Muungano lina Mamlaka Makubwa lakini ni dogo, Wabunge jumla ni 75, Ibara ya 113
(v) Utaratibu mzuri wa kuhakikisha kunakuwepo na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma soma ibara za 227, 228, 229 na 232
2. Muundo huu unaweza kuibua tatizo la uchangiaji gharama za uendeshaji wa muungano baina ya washirika;
Rejea Majibu ya Rasimu kwa suala hili hapa kwa ufupi;
(i)
Kwanza itambulike, suala la uchangiaji ni la Kikatiba, sio takwa la
mtu, utashi wa kiongozi au maamuzi ya Serikali ya Tanganyika au
Zanzibar. Ambaye atakataa kuchanga ama Rais wa Tanganyika au Zanzibar
anahatarisha uwepo wa mamlaka ya Jamhuri ya Muungano na anataka kutweza
mamlaka ya muungano, huyo ni
mhaini kwasababu aliapa kuutetea na kuudumisha Muungano, rejea Ibara ya 9, 69 na 88(2)(d)
(ii)
Masuala ya uchangiaji wa gharama za uendeshaji wa muungano, ni masuala
ya kiutaalamu, kiutendaji na kiuongozi. Masuala haya kimfumo
yataratibiwa na Tume ya Uhusiano na Uratibu rejea Ibara za 109, 110, 111
na 112
(iii)Ikumbukwe anayetunza akaunti za fedha za Nchi
Washirika ni Benki Kuu ya Jamhuri ya Muungano kupitia Benki za Serikali
za Nchi Washirika, rejea Ibara ya 233(1)(d) na isome pamoja na Ibara ya
234
(iv)Vyanzo vya Mapato vilivyo ainishwa na Rasimu
vinatosha Kabisa kukidhi mahitaji ya Jamhuri ya Muungano na Serikali
yake, Michango ni aina moja tu ya vyanzo, viko vyanzo vitano ambavyo kwa
tathmini ya Tume vinatosha kabisa, rejea Ibara ya 231
3. Muundo
huu unaweza ukasababisha uwepo wa sera zinazotofautiana au kukinzana
juu ya masuala ya msingi ya nchi na hivyo kuleta migogoro kati ya
Washirika wa Muungano au baina ya Washirika wa Muungano na Serikali ya
Muungano;
Rejea Majibu ya Rasimu hapa kama ifuatavyo;
(i)
Rasimu imefafanua, Mamlaka ya Serikali ya Muungano ambayo yako bayana
zaidi tofauti na sasa na hata pale Serikali ya Muungano ikitaka
kutekeleza jambo lililo chini ya mamlaka ya Serikali ya Tanganyika au
Zanzibar itafanyika hivyo kwa mujibu wa Katiba, rejea Ibara ya 62
(ii)
Rasimu inatoa maelekezo kwa Nchi washirika kuzingatia misingi ya
ushirikiano kwa haki na usawa kwa ajili ajili ya ustawi ulio bora wa
wananchi kutoka pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano rejea Ibara ya
65(1)
(iii)Rasimu imetatua changamoto tajwa hapo juu kwa
kuweka mfumo thabiti kikatiba ambao utakuwa na jukumu la kusimamia,
kuratibu na kuhakikisha kuna kuwiana kwa sera na sheria kwa mambo yasiyo
ya muungano, rejea Ibara ya 111(1)(b)
(iv)Rasimu pia
imeweka Misingi Mikuu ya Maendeleo ya Nchi ambayo inapaswa kuwa ndio
Dira ya Taifa na maelekezo kwa Mamlaka ya Nchi. Masuala ya Misingi na
Malengo ya Taifa (Dira) usimamizi na uratibu wake uko kitaifa, hapa
rejea Ibara za 10, 11, 111(1)(d) na 116
4. Kuna
uwezekano mkubwa kwa muundo huu kuleta tofauti za kimaendeleo baina ya
pande mbili za muungano kutokana na uwezekano wa kuwa na sera na mipango
tofauti. Uwezekano wa kuwa na tofauti kubwa za kiitikadi na utendaji
unaweza kuchangia hali hiyo.
Rejea Majibu ya Rasimu kama ifuatavyo;
(i)
Rasimu imetatua changamoto tajwa hapo juu kwa kuweka mfumo thabiti
kikatiba ambao utakuwa na jukumu la kusimamia, kuratibu na kuhakikisha
kuna kuwiana kwa sera na sheria kwa mambo yasiyo ya muungano, rejea
Ibara za 110 (a)(b)(c) na (d), 111(1)(a)(i)(ii), 111(1)(b) na 111(1)(d)
(ii)
Itikadi inaongozwa na Dira ya Taifa, ni dira ndio inasema ndoto za
wananchi na itikadi ni namna ya kufika huko ambako watanzania wanataka
kufika. Kidesturi itikadi huwa katika ngazi ya vyama vya siasa. Kwa mara
ya kwanza Rasimu inapendekeza Dira ya Taifa Katika Sura ya Pili ya
Rasimu ambayo ndio itakuwa ni maelekezo kwa Serikali (ya chama chochote)
na Mamlaka zote za nchi, rejea Ibara ya 10, 11, 111(1)(d) na 116
5. Muundo
wa Serikali tatu unaweza ukakuza hisia za utaifa (nationalistic
feelings) kwa Washirika wa Muungano na hivyo kufifisha Muungano na
kuhatarisha uwepo wake;
Rasimu ililitizama suala hili na yafuatayo ni majibu katika Rasimu;
(i)
Kwanza ifahamike kuwa, uraia ndio msingi mkuu wa uzalendo katika Nchi
yoyote. Kama ambavyo mamlaka ya nchi huwa na ukomo katika eneo la
kijiografia vivyo hivyo mamlaka ya nchi huwa na ukomo kwa watu
inaowajibika kwao, watu hawa hutambulika kwa mujibu wa sheria kama raia.
Utaifa wa mtu hujengwa katika uraia, Taifa la Tanzania litajengwa na
raia wa Tanzania. Rasimu imependekeza Uraia Mmoja na ni wa Jamhuri ya
Muungano na utapatikana kwa njia mbili, kuzaliwa na kujiandikisha, rejea
Ibara ya 56
(ii) Zanzibar na Tanganyika hazina raia wala
sio Mataifa, ni maeneo tu ambayo tumeyapa hadhi katika Rasimu ya “Nchi
Washirika” na ieleweke Nchi washirika sio Nchi kwa tafsiri ya Sheria za
Kimataifa na Rasimu yenyewe. Wanaokaa Tanganyika na Zanzibar sio
watanganyika wala sio wazanzibari bali ni wananchi wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania wanaoitwa “Watanzania”, rejea Ibara ya 64
(iii)Hisia
za utaifa huibuka pale ambapo historia na asili ya wale wanaoungana
inapofutwa. Uzoefu umeonesha kuwa kwa kufuta asili na historia ya
Tanganyika kwa makusudi ndio umekuwa mwiba mkubwa kwa utangamano na
umoja wa Jamhuri ya Muungano. Tanganyika imendelea kujifufua na
kujionesha katika nyanja zote kwa sura ya Jamhuri ya Muungano na kuiweka
kando Zanzibar kana kwamba ni ka-sehemu ka Tanganyika Mkuu. Salama yetu
ni kuiweka Tanganyika kwenye mwanga na kuiwekea masharti ya kikatiba
ambayo yataiongoza na kuifanya sehemu na eneo la Nchi Moja inayoitwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, rejea Ibara ya 64 na 65
(iv)Mwisho
wa siku Tanganyika na Zanzibar si Mataifa, si nchi na hazina raia,
Taifa ni Moja, Nchi ni Moja na Raia ni Wamoja na ni wa Nchi inayoitwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye Muundo wa Shirikisho lenye Mamlaka
kamili na lenye serikali tatu, rejea Ibara za 61, 63, 64, 65, 66, 67,
70, 71, 72, 110, 111,117, 119, 156 na 235
6. Muundo
huu unaweza ukaleta misuguano (paralysis and deadlocks in decision
making) katika kufanya maamuzi juu ya masuala magumu ya kitaifa.
Rasimu imelitizama suala hili na kuliwekea masuluhisho yafuatayo;
(i)
Rasimu imeweka mifumo na vyombo vya kikatiba vya kuhakikisha hakuna
misuguano na kwamba kuna fursa pana zaidi ya kufanya maamuzi kwa
kuzingatia majadiliano, maridhiano na muafaka kwa maslahi ya Taifa na
wananchi wa Tanzania. Rasimu inaanzisha Tume ya Uhusiano na Uratibu
ambayo ndani yake ina viongozi wakuu ambao wana jukumu ya kulitizama
taifa. Mwenyekiti wa Tume ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano,
wajumbe ni Rais wa Tanganyika, Rais wa Zanzibar, Mawaziri Wakaazi wa
Tanganyika na Zanzibar pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje. Utagundua kila
mtu anayeweza kuamua yupo, rejea Ibara ya 109
(ii) Kuna
njia rasmi na zisizo rasmi za kutatua migogoro au kuondoa misuguano
katika kufanya maamuzi na zimefafanuliwa bayana katika Rasimu Toleo la
Pili. Njia rasmi ni pamoja na Tume ya Uhusiano na Uratibu, lakini pia
iwapo majadiliano yatashindikana na ukatangazwa kuwa ni mgogoro basi
mgogoro huwa utapelekwa kwenye Mahakama ya Juu ya Jamhuri ya Muungano
ambayo uamuzi wake utakuwa ni wa mwisho, rejea Ibara za 111(1)(e),
111(2) na 156
(iii)Njia nyingine za kutatua migogoro na
kuondoa misuguano katika kufanya maamuzi kama Tume imeshindwa ni pamoja
na kumtumia Rais na Taasisi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano, rejea Ibara
za 71 na 72
(iv)Njia nyingine ni pamoja na Baraza la
Ulinzi na Usalama ambalo limepewa dhamana ya kuunganisha sera za ndani,
kushughulikia masuala ya ulinzi na usalama, rejea ibara ya 237 na 238.